Na Mwandishi Wetu
Ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani juu ya ujenzi wa Soko la Kibirizi kisasa imeanza kutekelezwa kwa Viongozi kuanza kutembelea na kujadili namna ujenzi huo utakavyotekelezwa sambamba na Ujenzi wa barabara inayopita katika eneo hilo
Akizungumza katika kikao kilichofanyika Leo Oktoba 27, 2022 katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Mhandisi kutoka Mamlaka ya Bandari (TPA) Makao makuu Eng. Twaha Msita amesema timu ya Wataalamu imekuja kwa lengo la kuangalia namna ujenzi wa soko hilo utakavyotekelezwa kama ilivyoahidiwa na Rais katika ziara yake aliyoifanya hivi karibuni Mkoani Kigoma
Amesema katika ziara yao wametembelea eneo la soko la Kibirizi ili kupata ukubwa wa eneo, uchoraji ramani na kupata mapendekezo ya gharama ya ujenzi ikiwa ni hatua ya awali kwa lengo la kuboresha Mazingira ya Wafanyabiashara na Wajasiriamali wa Soko hilo
Ameendelea kusema kukamilka kwa ujenzi wa Soko hilo kisasa utawanufaisha Wafanyabiashara walio wengi na biashara kufanyika katika nyakati zote ukilinganisha na sasa eneo hilo kujaa maji
Amesema miundombinu itakayojengwa katika Soko hilo ni pamoja na ujenzi wa Shedi za Wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi, Mabanda, Ujenzi wa Migahawa ya vyakula, Ujenzi wa vituo vya kupaki daladala, Bajaji na boda boda
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Evans Mdee amesema Manispaa hiyo inazingatia maagizo yaliyotolewa na Rais kwa kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Soko hilo kabla ya kuanza kwa mradi ili kuona namna watakavyoweza kupisha ujenzi huo
Amesema Wafanyabiashara na Wajasiriamali watakaopisha ujenzi huo watapewa kipaumbele pindi ujenzi utakapokuwa umekamilika
Amesema kuboreshwa kwa Soko hilo kwa ujenzi kisasa kutakuza Mapato ya Wafanyabiashara, kuvutia Wateja na Wafanyabiashara Wakubwa na kuongezeka kwa mapato ya Manispaa hiyo
Ahadi ya Ujenzi wa soko la Kibirizi Kisasa ilitolewa na Rais October 18, 2022 wakati akihutubia Wananchi waliojitokeza kumpokea eneo la Kibirizi mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika Ujenzi wa bandari ndogo ya Kibirizi
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa