Na Mwandishi Wetu
Kukamilika kwa zoezi la anwani za makazi kutarahisisha Serikali kufikisha huduma za maendeleo na manunuzi ya Kidigitali kwa Wananchi
Ameyasema hayo Mratibu wa zoezi la ukusanyaji wa anwani za Makazi Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Haji Omary Mwilima leo Februari 22, 2022 alipokuwa katika kipindi cha #Goodmorning Kigoma kinachorushwa kila siku asubuhi na Radio joy 90.5
Mratibu huyo amesema kukamilika kwa zoezi hili kutafanya Serikali kuwa na takwimu sahihi ya maeneo yanayohitaji huduma za kijamii kama vile afya, elimu, na miundombinu mbalimbali ambazo Wananchi wa eneo husika wanahitaji ikiwa ni pamoja na kurahisisha upelekaji wa huduma hizo
Ameendelea kusema kukamilika kwa zoezi hilo kila Mtanzania atakuwa na anwani halisi ya Makazi yatakayosaidia kila mtu kupatikana kirahisi, utambulisho wa watu, usajili wa biashara na mali na kuboreshwa kwa taarifa ya vizazi na vifo katika jamii
Kukamilika kwa zoezi hilo pia kutusaidia kufanyika kwa biashara mtandaoni ambapo Wafanyabiashara na wanunuzi watakuwa na uwezo wa kununua na kumfikishia mteja bidhaa, upatikanaji wa huduma za dharura kama vile polisi, huduma za zima moto kwa uharaka kutokana na uwepo wa anwani na taarifa kamili za kila mtu
Amesema zoezi hilo litafanyika kwa kutoa namba ya anwani ( namba ya jengo, au kiwanja), majina ya barabara au kitongoji na postikodi
Aidha ameendelea kusema hadi sasa tayari Makundi mbalimbali yamepata mafunzo ya namna zoezi hilo litakavyofanyika wakiwemo Madiwani, Watendaji kata na Mitaa na uelimishaji huo unatarajia kufanyika kwa Wenyeviti wa Mitaa na vijana watakaohusika katika zoezi hilo
Amehitimisha kwa kuwataka Wananchi, Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano wa watakaokuwa wakikusanya taarifa hizo wakishirikiana na viongozi wa kata na mtaa
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa