Na mwandishi wetu
Manispaa ya Kigoma/Ujiji leo march 16, imeanza kutoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona katika taasisi za shule kwa Walimu na Wanafunzi kutokana na ugonjwa huo kuenea kwa kasi katika nchi mbalimbali duniani
Wataalamu kutoka idara ya afya ya manispaa hiyo wametoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona kwa shule 5 za msingi na sekondari ambapo pia walimu wakuu wa shule zote za msingi, walimu wa afya mashuleni na waratibu Elimu kata wamepata elimu hiyo
Wakiwa katika uelimishaji huo Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dk Siwale amewataka walimu na wanafunzi kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kuepuka baadhi ya matendo yaliyozoeleka katika jamii kama kusalimiana kwa kupeana mikono na kukumbatiana
Aidha Mganga Mkuu huyo amesema ugonjwa huo kwa sasa hauna chanjo wala tiba ya moja kwa moja , na matibabu yanayofanyika ni kwa kuzingatia dalili zinazojitokeza na ufuatiliaji kwa ukaribu na ugonjwa huo huambukizwa kwa njia ya hewa au kugusa majimaji au kamasi kutoka kwa mtu mwenye virusi vya korona
Naye Dk Shabani Magorwa amesema dalili za ugonjwa huo wa corona ni kukohoa, homa kali, kuumwa kichwa, mwili kuchoka, vidonda kooni, maumivu ya misuli, na kupumua kwa shida hali inayoweza kupelekea umaiti kwa mtu mwenye dalili hizo
Amewataka walimu kuwa makini na wanafunzi wao kwa kuwataka kunawa mara kwa mara baada ya kushika na kugusa kitu chochote na kuwataka walimu kutoa taarifa mara baada ya kuona mtu mwenye dalili hizo ili kuweza kupewa huduma mara moja na timu iliyoandaliwa manispaa ya Kigoma/Ujiji
Aidha Mganga mkuu huyo amewataka walimu kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wanafunzi na walimu wengine ambao hawakupata elimu hiyo na hatimaye elimu hiyo kuifikia jamii kwa kila mmoja kuwa barozi wa utoaji elimu hiyo
Naye Kaimu Afisa elimu wa Manispaa hiyo Bi. Gunaguje ameshukuru elimu hiyo iliyotolewa na wataalamu kutoka idara ya afya na kusema maelekezo yaliyotolewa watayasimamia na kuhakikisha kila shule inakuwa na vyombo vya usafi vya unawaji katika shule zote na kusema kupitia elimu hiyo iliyotolewa kwa walimu na wanafunzi jamii kubwa ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji itatolewa na kwa watu wengine
Nao baadhi ya walimu waliohudhulia katika elimu hiyo akiwemo Madamu Suzana na mwalimu Julius Zackaria wameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa kuratibu elimu hiyo kwa lengo la tahadhari la ugonjwa huo wa Corona
Nao wanafunzi wa shule ya sekondari Bishop Kahurananga Godfrey Danga na Suzana Elikana wameshukuru wataalamu hao kwa kuwapelekea elimu hiyo huku wakisema maelekezo waliyopata namna ya kujikinga na ugonjwa huo watayafanyia kazi na kuwa mabalozi kwa wanafunzi wengine na jamii yote kwa ujumla
Mganga mkuu wa Manispaa hiyo amehitimisha kwa kuwashukuru walimu, wanafunzi na waratibu elimu kata kwa kuonesha ushirikiano wao na kusema elimu hiyo waliyoianza kuitoa ni endelevu ili kupambana na ugonjwa huo wa Corona kwa kata zote, mitaa na itafanyika katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kama vile sokoni, mashuleni na maeneo ya starehe
Tayari Manispaa ya Kigoma/Ujiji imeshaanda eneo na wataalamu wa kuwahudumia wagonjwa hao kwa kuwapatia mafunzo endapo mgonjwa wa Ugonjwa huo atagundulika kuwepo, Na tayari vifo 3,217 vimelipotiwa nchini China huku vifo 1,809 nchini Italia Tangu ugonjwa huo kugundulika
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa