Mratibu wa jamii na mazingira katika mradi wa uendeleaji miji ya kimkakati Tanzania au Tanzania Strategic Cities Project (TSCP) katika manispaa ya Kigoma/Ujiji bi. Agnes Sanga jana Agosti 23, amewataka wananchi wa mtaa wa ujenzi manispaa ya Kigoma Ujiji kutunza miundo ya barabara inayotarajiwa kujengwa hivi karibuni.
Ameyasema hayo katika mkutano uliofanyika katika soko la Nazarethi katika kutambulisha mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ya Nazarethi yenye km 1.7 , katika mkutano huo wataalamu mbalimbali kutoka ofsi ya Mkurugenzi wa manispaa walihudhulia akiwemo Afisa malalamiko, afisa maendeleo ya Jamii na mratibu wa masuala ya UKIMWI manispaa ya Kigoma Ujiji, afisa mtendaji wa mtaa na wanakamati ya malalamiko ya kata na mtaa.
Akiendelea kuongea katika mkutano huo mratibu wa jamii na mazingira bi. Agnes Sanga amesema mradi huo unafadhiliwa na benki ya dunia na fedha zinazoletwa ni sehemu ya mkopo kwa wananchi hivyo wananchi hawana budi kuipenda miradi hiyo na kuweka mikakati mizuri ya kuweza kuitunza.
Mratibu huyo aliendelea kusema katika miradi hiyo inayotarajiwa kujengwa ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha usalama unakuwepo katika kipindi chote cha ujenzi wa barabara hiyo kwa kuhakikisha alama za usalama zipo katika maeneo yanayojengwa ili kuepuka ajali zinazoweza kujitokeza kwa kutoa taarifa katika ofsi za kata pindi wanapoona wajenzi hawakuweka alama hizo.
Aliendelea kuwataka wakazi wa mitaa hiyo kuhakikisha wanatunza mazingira na kuwa wasafi katika kipindi chote cha ujenzi na hata ujenzi utakapokuwa umekamilika kwa kuhakikisha mitalo inakuwa safi na kutotupa taka ovyo.
Lakini pia mratibu huyo aligusia suala la ajira kwa vijana , ambapo aliwataka vijana kuchangamkia suala la ajira kwa kuomba kufanya kazi zile zinzohusisha taaluma hata zile zinazotumia nguvu na kuacha kukaa vijiweni , alionya suala la ajira kwa watoto wadogo na kuwataka wakazi wa mtaa huo kuwa makini na suala la kuajiri watoto wadogo jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi na kusema endapo suala hilo litajitokeza wananchi wahakikishe wanachukua hatua kwa kutoa taarifa katika uongozi wa eneo husika.
Naye afisa malalamiko wa halmashauri Ndugu. Meleji Mollel akiwa katika mkutano huo aliweza kutambulisha kamati ya malalamiko ya mtaa na kata kwa wakazi na kusema tayari kamati hiyo ipo kazini na yapo malalamiko ambayo tayari wameanza kufanyia kazi yakiwemo ya kukatwa kwa bomba la maji katika kazi za awali za wakandarsi ambazo wamekwishaanza nazo.
Afisa malalamiko huyo alisema katika kipindi cha ujenzi yataweza kutokea matatizo tofauti tofauti ambayo yatahitaji utatuzi , alisema ni bora matatizo hayo yafuate hatua kwa hatua kuanzia ngazi ya mtaa, kata hadi kufikia manispaa kwa lengo la kutatuliwa
Lakini pia afisa huyo aliendelea kusema malalamiko wanayoshugulikia ni ya pande zote si upande wa wananchi bali pia hata kwa wakandarasi wanaojenga barabara hizo kwani yapo matatizo mengi yanayosabaibishwa na wanachi katika ujenzi ikiwemo wizi wa simenti, matusi hata ugomvi kwa wakandarsi kwa watu wasiowavumilivu.
Naye mratibu wa Ukimwi katika mradi huo wa TSCP aliwataka wakazi wa mitaa hiyo kuwa na uhusiano mzuri na wageni watakokuja kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo lakini pia kuwa makini na mahusiano yatakayojengwa ambayo hayataweza kuleta athari za magonjwa ya zinaa na UKIMWI.
Aliendelea kusema kama mjenzi au mkandarsi anaweza kupendana na mwenyeji wa eneo hilo ni muhimu kufuata hatua za kupima kabla ya kushiriki tendo la ndoa na kuwataka pia kuweza kutumia kondomu kwa ajili ya kuzuia maambukizi hayo ya virusi vya Ukimwi.
Naye afisa maendeleo Ndugu. Radan Lameck akiwa katika mkutano huo alisema ni fursa nzuri ya kimaendelea iliyojitokeza katika ujenzi wa barabara hiyo kwani itaweza kuleta mapinduzi chanya ya kimaendeleo ikiwa ni kuongeza thamani ya ardhi pamoja na makazi .
Aliendelea kusema wakazi wa manispaa wachangamkie fursa hiyo katika kufatilia ujenzi wa barabara yenye ubora ili bara bara iwe imara kwani itaweza kusaidia madereva wa bodaboda na magari kuokoa fedha nyingi za matengenezo kwa kupita katika barabara iliyo imara.
Nao wananchi wa mtaa huo wa ujenzi wakiwa katika mkutano akiwepo Ndugu. Mussa Hamisi na Yaredi Bada wameweza kupongeza kwa mkutano uliofanyika kwa kusema wamepata elimu ya kutosha juu ya mradi huo wa barabara unaojengwa na kuomba ajira zitakazotolewa zisije kutolewa kwa upendeleo wa aiona yeyote kwa wakazi wa eneo hilo.
Naye mratibu wa jamii na mazingira bi. Agnes Sanga amehitimisha kwa kuwashukuru wakazi wa mtaa huo kwa kuweza kujitokeza katika mkutano huo na kusema tayari wakandarasi wapo katika miradi na wameanza ujenzi hivyo wananchi watoe ushirikiano katika mradi huo wa barabara unaojengwa kwani mradi huo na barabara zingine zikiwemo ambazo ni barabara ya kakolwa , barabara ya kitambe mwembetongwa, barabara ya Burega, barabara ya Kagera pamoja na mfereji wa mlole na katonyanga yote itajengwa kwa mwaka mmoja na miezi mitatu.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa