Na Mwandishi wetu
Mapema leo Septemba 19, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dr. John Pombe Magufuli amepokea ugeni wa Rais wa Burundi Mhe. Evaristi Ndayishimiye Mkoani Kigoma katika Uwanja wa mpira wa Lake Tanganyika uliopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji
Katika Mapokezi hayo Rais wa Nchi ya Burundi alikagua kikosi cha Gwalide cha Jeshi na kupigiwa mizinga ishirini na moja akiwa na mwenyeji wake Raisi wa Nchi hiyo, baadhi ya Mawaziri wa Serikali zote mbili , Viongozi wa vyama vya kisiasa na Wananchi wa Mkoani Kigoma waliojitokeza katika Mapokezi hayo
Akihutubia Mkutano huo Rais wa Burundi amempongeza Rais wa Tanzania Mhe Dr. John Pombe Magufuli kwa namna anavyowatumikia Watanzania na kusema yeye kama kiongozi amevutiwa namna Rais huyo anavyowatumikia Watanzania huku Akisema Rais Magufuli anamchukulia kama baba yake wa Uongozi na amekuja kujifunza kwake
Aidha Rais huyo wa Burundi amempongeza Raisi wa Tanzania kwa kuikuza Kigoma kwa ujenzi wa Miundombinu kama vile Barabara za mtaani, Ujenzi wa Bandari ya Nchi Kavu na Ujenzi wa Mahakama huku akisema Miundo mbinu hiyo itaibadilisha Kigoma katika nyanja za kiuchumi kwa Wananchi wake
Ameendelea kumpongeza Rais Magufuli kwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kuijenga Tanzania kwa Ujumla huku akisema Ujenzi wa Reli ya Kisasa hautainufaisha Tanzania Tu bali pia na Nchini Burundi na Jumuia ya Afrika Mashariki kwa Usafirishaji wa Bidhaa mbalimbali
Amehitimisha kwa kusema " Kwa sasa Nchini Burundi hali ya Usalama ni shwari , tumekaa pamoja tukaona Burundi hakuna Mtusi wala Mhutu Wote ni Warundi na tunaongea Kirundi Na Wakoloni ndio waliotugawa tu na hatutaki kurudia machafuko kama yale ya zamani Maana tunajua Burundi ikiwa na Furaha na Kigoma inafuraha maana tuliwasumbua kwa wakimbizi"
Naye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dr. John Pombe Magufuli akimkaribisha Raisi huyo Wa Burundi amesema uhusiano wa kibiashara kwa Nchi hizo mbili umekuwa kutoka Tsh billion 115.15 mwaka 2016 hadi hivi sasa kufikia Tsh billion 201
Ameendelea kusema uhusiano umeendelea kukua ambapo wawekezaji na wafanyabiashara wameendelea kushirikiana ambapo zaidi ya Kampuni kumi za Watanzania zinaendelea na Biashara katika Nchi ya Burundi
Amesema asilimia tisini na tano (95%) bidhaa za Burundi zinapita katika bandari ya Dar es salaam na kwa mwaka 2019 Tani 481,000 zilisafirishwa kwenda Nchini Burundi kupitia bandari hiyo
Raisi Magufuli ameeleza mambo watakayoyazungumza na Rais huyo wa Burundi ikiwa ni kuendelea kuboresha Mazingira ya kibiashara baina ya Nchi hizo huku akisema watajadiliana Madini na dhahabu za Burundi kuja kuuziwa Mkoani Kigoma ikiwa ni eneo la soko la bidhaa hizo
Ujenzi wa mtambo wa kuchenjua Madini baina ya Nchi hizo mbili, na safari za Anga zikiwa sehemu ya Mazungumzo ambapo mpango wa Ndege zinazotua Mkoani Kigoma kwenda hadi Mji wa Bunjumbula Nchini Burundi
Aidha Rais Magufuli amehitimisha kwa kuweka wazi mpango wa Ujenzi wa Meli mpya mbili, Mkoani Kigoma zitakazotumika Katika Ziwa Tanganyika moja itakayokuwa na uwezo wa kusafirisha abilia zaidi ya mia sita na meli moja ya Mizigo, huku meli zingine mbili ikiwemo Mv Liemba kukarabatiwa ili kukuza Sekta ya Biashara baina ya Nchi hizo na kuendelea kupanua uwanja wa Ndege ulilopo Mkoani hapo
Katika ziara ya Raisi wa Burundi, Rais Magufuli amezindua Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania lililojengwa Mkoani Kigoma kwa fedha za ndania mbapo litasaidia kupunguza Usumbufu na gharama kwa Wakazi wa Mkoa huo ambapo awali Wakazi wa Mkoa huo walikuwa wakisafiri kwenda Mkoani Tabora Aidha Rais wa Burundi Mhe Evaristi Ndayishimiye amefanya ziara hiyo Nchini Tanzania ikiwa ni ziara yake ya Kwanza Tangu Kuchaguliwa Nchini kwake, Huku akisisitiza kuwa lengo la ziara yake hiyo ni kuja kujifunza namna Rais Magufuli anavyofanya kazi na Kuwatumikia Watanzania ili imsaidie na yeye katika kipindi chake cha Utawala
PICHA NA MATUKIO ZAIDI TEMBELEA www.kigomaujijimc.go.tz
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa