Na Mwandishi wetu
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji wamehitimisha sherehe za kuazimisha miaka arobaini na tatu ya chama hicho kwa kushiriki shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa tisa (9) unaoendelea katika sekondari ya Gungu iliyopo katika halmashauri hiyo
Wanachama hao wamewasili katika eneo hilo la Shule mapema asubuhi ya leo Wanaume kwa Wanawake wakiwa wamevalia sare zao za Chama huku baadhi wakiwa na vifaa vya Ujenzi, wengine wakija kushiriki katika kusogeza tofali na mawe kwa mafundi wanaoendelea na ujenzi huo
Akiwa katika eneo la kazi Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya Ndugu. Alhaji Yasini Mtalikwa amesema katika kuhitimisha sherehe za miaka 43 ya kuanzishwa kwa Chama Cha Mapinduzi wanachama na viongozi wa chama hicho wameamua kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji katika zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa 38 unaoendelea katika Halmashauri hiyo
Ameendelea kusema Chama Cha Mapinduzi (CCM) wajibu wake ni kusimamia Serikali na kuhakikisha miradi ya Maendeleo inasonga mbele na kuinufaisha jamii inayoizunguka , huku miradi hiyo ikiwa katika hali ya ubora na viwango vinavyositahili
Amesema “ Chama na Wanachama lazima nao waunge juhudi za viongozi wa serikali kwa hali na mali ili kuhakikisha Ilani ya Chama Tawala inatekelezwa kwa maslahi ya wananchi wa Kigoma/Ujiji na Tanzania kwa Ujumla”
Amehitimisha kwa kusema zoezi hili liliofanyika leo katika kushiriki Ujenzi wa vyumba vya madarasa ni mwendelezo wa kushiriki shughuli zingine za kijamii katika idara na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali ikionesha ni namna gani Chama na Serikali inafanya kazi pamoja ili kuifikia malengo ya Taifa
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Masanga ambapo shule hiyo ipo Mhe. Charles William amewapongeza Wanachama wa Chama hicho kwa kushiriki ujenzi wa shule hiyo unaoendelea na kusema ujenzi huo ulatela tija kwa jamii na kuhakikisha unamaliza tatizo la uwepo wa watoto mtaani kutokana na uwepo wa miundombinu mashuleni ikiwa ni fursa kwa vijana kufikia malengo yao kupitia elimu watakayoipata
Ameendelea kusema katika kuhakikisha madarasa hayo yanajengwa na kukamilika wakaazi wa Kata ya Gungu wameazimia kila kaya kuchangia kiasi cha fedha shilingi elfu kumi na kusema kiwango hicho kitatosha katika ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa hayo, na wanafunzi waliokosa nafasi kwa upungufu wa vyumba vya madarasa kuanza masomo yao mapema mwezi marchi
Naye Mkuu wa Idara ya Mipango na Uchumi katika Manispaa hiyo Ndugu. Ferdnand Filimbi kwa niaba ya Mkurugenzi amewapongeza wanachama wa chama hicho kwa kufikia miaka 43 ya chama hicho huku akishukuru wanachama hao na viongozi wao kushiriki katika ujenzi wa madarasa hayo tisa (9) kwa shule ya sekondari Gungu
Ameendelea kusema ukosefu wa vyumba vya madarasa kwa halmashauri kwa mwaka huu imekuwa tatizo na kufanya baadhi ya wanafunzi waliofaulu kushindwa kulipoti kwa wakati na kusema tatizo hilo tayari limewekewa mikakati ya ujenzi wa madarasa mapema na kuwa mpango endelevu na kuanzia mwezi wa tano Ofisi za kata zimepewa agizo la kuwa na benki ya tofali laki moja na kuweka mikakati ya kupata kiti, meza,na madawati kwa shule zilizopo
Naye afisa elimu wa sekondari Ndugu. Kajanja amesema hatua hiyo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa italeta hali nzuri ya ufundishaji na ujifunzaji kwa Walimu kuwafikia Wanafunzi kwa mahitaji ya mmoja mmoja na kuboresha suala la ufaulu kwa wanafunzi hao
Ameendelea kusema kwa kawaida wanafunzi wanatakiwa kila darasa kuwa na wanafunzi arobaini (40) na isiyozidi arobaini na tano (45) ili wanafunzi wajifunze katika mazingira salama na yenye mvuto na mwalimu kuwahudumia wanafunzi wake pasipo msongamano
Mmoja wa wanachi wa kata ya Gungu Bi. Mwamini Hamisi amesema chama cha Mapinduzi kimefanya jambo jema katika kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa na kuboresha elimu kwa wanafunzi wanaosoma kwa shule zilizopo katika halmashauri hiyo huku akitoa wito kwa vyama vingine vya kisiasa kuiga kile kilichotendwa na chama hicho tawala.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa