Na Mwandishi Wetu
Siku kumi na sita (16) za kupinga ukatili wa Kijinsia zimeanza kuadhimishwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa kutoa elimu na kuzijengea uwezo Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ngazi ya kata kwa lengo la kupambana na vitendo vya ukatili ndani ya jamii
Mabaraza hayo ya Usuluhishi yameanza kujengewa uwezo Juzi Novemba 25, na 26, 2021 Manispaa ya kigoma/Ujiji katika Kata Kipampa, Buzebazeba, Rusimbi na Kata ya Majengo ambapo elimu hiyo imetolewa na Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii , Maafisa wa Jeshi la Polisi dawati la Jinsia, Wasaidizi Wa Kisheria, Viongozi wa dini na huku mafunzo hayo yakifadhiliwa na Mradi wa BAKAID wa kupambana na kupinga ukatili wa Kijinsia unaofadhiliwa na Shirika la Norwegian Church Aid (NCA)
Afisa Maendeleo ya Jamii Ndugu. Jabir Majira wakati wa kuzijengea uwezo mabaraza ya Usuluhishi ngazi ya kata
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya kigoma/Ujiji Ndugu. Jabir Majira aliyataka Mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ngazi ya kata kuendelea kutatua changamoto za ukatili ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa kutoa elimu katika mikutano ya Wananchi na Maeneo mengine yenye mikusanyiko ya Watu kupinga vya ubakaji, kuwatumikisha Watoto kazi ngumu, kutowapeleka watoto Shule na unyanyasaji wa kuwanyima fursa Wanawake kujiingizia kipato
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia Bi.Anastasia Daudi aliyataka Baraza hayo kuelimisha Jamii kusimamia Malezi ya familia na kuripoti vitendo vya ukatili vinavyojitokeza na kutoa ushirikiano katika kushughulikia vitendo hivyo kwa Uongozi na Viongozi wa Mtaa, Kata, Ustawi wa jamii, Jeshi la Polisi kutokana na athari za vitendo hivyo
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia Bi.Anastasia Daudi
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia Bi.Anastasia Daudi mradi wa wa kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia kutoka BAKAID Kigoma Ndugu. Juma Bewa aliwataka Maafisa Watendaji Kata na Mtaa kuhakikisha katika vikao na Mikutano ya Wananchi elimu ya kupinga vitendo vya ukatili inatolewa kila mara na kuweka kauli mbiu ya eneo husika ya kupinga vitendo hivyo ili jamii zipate kuwa salama
Aidha alisema Shirika la BAKAID katika maadhimisho ya Mwaka huu imepanga kutoa elimu Manispaa Kigoma/Ujiji ya kupinga vitendo vya Ukatili katika Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ngazi ya kata, Mashuleni , Viongozi wa dini na kuendeleea kutoa elimu hiyo Wilayani Uvinza katika Vijiji vya Kazuramimba na Kandaga kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Serikalini kama vile Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na Maafisa wa dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi, Viongozi wa Kimila na Viongozi wa dini Mbalimbali
Afisa Mtendaji wa Kata ya Rusimbi aliwapongeza Shirika la BAKAID kwa kuzijengea Uwezo, mafunzo na elimu ya kupambana na vitendo vya Ukatili Mabaraza ya Usuluhishi wa migogoro huku akisema wameendelea kupambana na vitendo na viashiria vya ukatili ambapo tayari kikundi cha Malezi chanya kwa Watoto kimeundwa na tayari wameweza Kuwarejesha kwa wazazi watoto ambao wamekuwa wakilala Mitaani, kutatua Migogoro ya Wanandoa, na kutoa elimu kwa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakitumia madawa ya kulevya
Tayari maadhimisho hayo Kitaifa yamezinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Novemba 25, 2021 katika ukumbi wa mikutano Mlimani City jijini Dar es salaam na yanatarajiwa kuhitimishwa Desemba 10, 2021 yakiwa na kauli mbiu " Ewe Mwananchi, Komesha ukatili wa Kijinsia sasa"
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa