Manispaa ya Kigoma/Ujiji imeendelea kuadhimisha siku kumi na sita (16) za kupinga ukatili wa Kinjisia kwa kutoa elimu kwa vikundi vya wajasiriamali ikiwemo Wanawake na Vijana
Siku ya Ijumaa Novemba 26, 2021 Maafisa Maendeleo ya Jamii wakiambatana na Wataalamu kutoka Ofisi ya BAKAID-Kigoma chini ya Ufadhili wa Shirika la Norwegian Church Aid (NCA). walitembelea na kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili katika kikundi cha Wajasiriamali Wanawake kilichopo kata ya Kasimbu (kikundi cha Huruma) wanaojishughilisha na Ushonaji shuka, Kilimo cha Bustani , Utengenezaji wa Sabuni za Maji na Miche
Wanachama wa Kikundi hicho walitakiwa kutovumilia na kuficha vitendo vya ukatili vinavyofanyika kwenye ndoa na familia , na kutoa taarifa katika vyombo vya kupinga unyanyasaji huo kama vile Dawati la Jinsia jeshi la Polisi, Ofisi za Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Mtendaji Kata na Mtaa ili kuepukana na athari za vitendo hivyo kama vile vifo, udhalilishaji na chuki
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Majira Jabir akifafanua aina za ukatili alisema Upo ukatili wa kihisia kama kuwatukana Watu kwa maneno ya udhalilishaji , ukatili wa Kibaguzi ambapo baadhi ya watoto katika familia hupewa kazi kubwa na nyingi ukilinganisha na umri wao, ukatili wa vipigo, na ukatili wa Kiuchumi ambapo Mwanaume au mwanamke humkataza mmoja wapo kujishughulisha uzalishaji mali pasipo sababu yeyote
Mwanasheria na Wakili kutoka Shirika la Norwegian Church Aid (NCA) Bi. Rosalia Ntirihungwa alisema ni kosa kisheria kwa watoto wadogo chini ya Umri wa Miaka kumi na nane (18) kuingizwa na kulazimishwa kuoa au kuolewa kwa Lengo la kujipatia kipato kwa wazazi au walezi
Aidha aliendelea kuwataka wazazi na walezi kuendelea kuimalisha ulinzi kwa watoto na kuhakikisha wanapata Mahitaji Mhimu ikiwa ni pamoja kuwapeleka shule kwa lengo la kujipatia elimu
Afisa Mradi wa kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia kutoka BAKAID Kigoma Ndugu. Juma Bewa alisema elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali kwa lengo la kutokomeza vitendo hivyo vya ukatili katika Manispaa hiyo
Elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili imeendelea kutolewa Leo Novemba 29, 2021 kwa makundi mbalimbali kama vile Madereva boda boda na tax katika Kata ya Gungu na Kibirizi, na kwa Mwaka huu maadhimisho haya Kitaifa yana kauli mbiu " Ewe Mwananchi, Komesha ukatili wa Kijinsia sasa"
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa