Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga leo March 30, amekemea suala la wazazi kuwachia huru watoto kutembea ovyo masokoni na mtaani baada ya kufunga shule ili kujikinga na ugonjwa wa Corona huku akiagiza watoto hao kukamatwa na wazazi wao kulipishwa faini
Ameyasema hayo katika ziara aliyoifanya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ya kutembelea maeneo yenye mikusanyiko ya watu sokoni na katika hoteli ili kujiridhisha hatua zilizochukuliwa ili kujikinga na ugonjwa huo wa Corona kwa wakazi wa Manispaa hiyo
Akiwa katika soko la Buzebazeba amesema “tumefunga shule ili wanafunzi waweze kutulia majumbani ili kujikinga na Ugonjwa wa Corona sasa imekuwa fursa ya watoto hao kutembea ovyo Masokoni, na kutumwa na wazazi wao kwa lengo la kufanya biashara , Nasema Jambo hili halikubariki lazima wazazi tuwachukulie hatua kali”
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kufanya oparesheni ya kuwakamata watoto wanaotembea ovyo masokoni ili kuweza kuwafanyia mahojiano kwa lengo la wazazi wao kutozwa faini au kufikishwa katika vyombo vya kisheria
Aidha mkuu huyo wa Mkoa amewataka wafanya biashara kuweka utaratibu mzuri kutoweka msongamano katika kila duka au bidhaa bali kuwe na mda wa kupeana nafasi kati ya mteja na mteja ili kuweza kujilinda na virusi vya Corona vinavyoweza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kugusana
Amewataka wanunuzi wa bidhaa masokoni kutohemea kila mara bali wanunue chakula na mahitaji mengi zaidi kwa lengo la kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima na kuhakikisha kunawa kila wanapotaka kuingia katika masoko
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo masoko yote ya halmashauri kufungwa kwa mabomba ya maji ili maji kupatikana mda wote kwa lengo la kuendeleza usafi wa kunawa mikono kila mara ili kujikinga na ugonjwa huo
Naye mganga mkuu wa Mkoa Dr. Chacha ametoa ushauri kwa wameliki wa hoteli kuhakikisha wanajiridhisha na wageni wanaokuwa wanaingia kupata huduma na kufuata taratibu zote za kuwahakiki ikiwepo usajili wa wageni hao na kutoa taarifa pale mtu anapoonesha dalili tofauti tofauti za Ugonjwa wa Corona’
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu Mwailwa Pangani amesema tayari elimu imeshatolewa kwa wananchi kupitia makundi mbalimbali na taasisi za serikali na zisizo za serikali katika kuhakikisha wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji wanakuwa tayari kupambana na ugonjwa wa Corona
Naye mwenyekiti wa wafanya biashara Soko la Buzebazeba Ndugu. Amrani Abduli ameipongeza Ofisi ya mkuu wa Mkoa kwa kutembelea masoko na kusema elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Corona tayari wameshaipata kupitia wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji hatua na njia za kujikinga na ugonjwa huo
Katika ziara iliyofanyika mkuu wa mkoa amekataza mikusanyiko ambapo maeneo yaliyotembelea ni soko la Buzebazeba, soko la Mwanga, Soko la dagaa Kibirizi, Lake Tanganyika Hotel, Green view Hotel, Hill top Hoteli na eneo la Bangwe Beach
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa