Na Mwandishi Wetu
Zoezi la Anwani za Makazi Manispaa ya Kigoma ilizinduliwa Mapema February 09, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Ndugu. Thobias Adengenye ambapo zoezi hilo liliendelea kwa hatua mbalimbali za utekelezaji
Mara baada ya Uzinduzi huo makundi ya Wataalamu na viongozi wa Kisiasa walipewa elimu na mafunzo namna zoezi hilo litakavyofanyika na kuwanufaisha wakazi wa Manispaa hiyo na Watanzania Wote
Makundi yaliyopatiwa elimu kwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji ni pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kigoma, Waheshimiwa Madiwani, Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi mbalimbali, Wakuu wa idara na Vitengo, Watendaji Kata na Mitaa, Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za Mitaa, Makundi ya wajasiriamali, Wataalamu wa Ukusanyaji Taarifa na Wananchi wote kupitia vyombo vya habari vilivyopo katika Manispaa hiyo
Zoezi la Anwani za makazi linaloendelea linahusisha uchukuaji taarifa, Utambuzi na uwekaji wa Anwani za makazi ambapo unafanyika kwa kutoa namba ya anwani (namba ya jengo, au kiwanja), majina ya barabara au kitongoji na postikodi
Aidha katika zoezi hilo anwani za makazi, taasisi, na Maeneo ya Umma zaidi ya elfu arobaini na saba (47,000) zimetambuliwa na Wataalamu waliopata mafunzo na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa vijana zaidi ya mia moja na ishirini (120) katika ukusanyaji taarifa na uandishi wa namba
Aidha makundi mbalimbali ya Wajasiriamali na mafundi wa kuchomelea wanaendelea na shughuli ya uzalishaji wa namba za Anwani ambapo hadi sasa Kikundi cha vijana Talanta kilichopo Kata ya Buzebazeba eneo la Burega na makundi mengine ya Wajasiriamali wanaendelea na uzalishaji huku zaidi ya namba za Anwani Mia saba (700) tayari zimesambazwa katika Ofisi za Kata na Mitaa na kiasi cha fedha Million kumi na tatu (Tsh 13, 000,000) kinatarajia kitumika katika zoezi hilo
Katika Mitaa sitini na nane (68) iliyopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji zaidi ya vijana mia mbili (200) wanatarajia kunufaika na ajira za ubandikaji wa vibao katika makazi, taasisi na maeneo ya umma kutokana na ajira ambazo Watendaji wa Mitaa hiyo watazitoa kwa wakazi husika
Kazi nyingine inayoendelea kwa makundi ya wajasiriamali ni uzalishaji wa nguzo na vibao vya majina ya barabara ambapo zaidi ya barabara elfu mbili mia moja tisini na saba (2197) zinatarajiwa kuwekwa miundombinu hiyo mwanzo na mwisho mwa barabara husika na zaidi ya vijana sabini ( 70) wananufaika na uzalishaji wa miundombinu hiyo
Aidha kukamilika kwa zoezi hili kutaendelea kuwanufaisha kiuchumi wafanyabiashara, Wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni kwa kufanya biashara Mtandaoni kwa kutangaza bidhaa na kuwafikisha wateja kirahisi ikiwa ni pamoja na ufikishaji wa vifurushi
Faida zingine za kukamilika kwa anwani za makazi kutasaidia kila mtu anayeishi Nchini Tanzania kuwa na anwani halisi ya makazi, utambulisho wa watu wanaoishi katika maeneo husika, usajili wa mali, biashara, na kuboreshwa kwa usajili wa vizazi na vifo, ufikishaji wa huduma za maendeleo kwa wananchi kulingana na mahitaji yao, Huduma za dharura, kama vile polisi, zimamoto na magari ya wagonjwa, zinaweza kutambua maeneo yenye dharura na kuyafikia kwa haraka
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa