Na mwandishi wetu
March 17,2021 itabaki siku ya kihistoria katika vichwa vya Watanzania wengi wa Ndani na nje ya Nchi baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutangaza kifo cha Rais wa Tanzania Mhe. Dr John Pombe Magufuli
Makamu wa Rais(kabla ya kuapishwa kuwa Rais) huyo akitangaza Kifo hicho alisema Rais Magufuli alifariki majira ya saa kumi na mbili jioni siku hiyo akiwa katika hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es salaam alipokuwa akipatiwa matibabu kwa maradhi ya moyo aliyokuwa akisumbuliwa kwa zaidi ya miaka kumi hali ambayo ilileta mshituko na simanzi kubwa kwa Watanzania na raia wa Nchi zingine
kwa hakika Rais na Mhe. Dr John Pombe Magufuli alikuwa ni kiongozi aliyependa maendeleo ya Watanzania wote hasa walio wachini ambapo yeye aliwaita Wanyonge hali ambayo ilimfanya kupendwa na wananchi wa ndani ya Nchi na wa Mataifa mengine kutokana na namna alivyokuwa akitatua kero na vilio vya wananchi hao
Ni kiongozi aliyependa kuona matokeo makubwa katika utendaji kazi kwa viongozi wa Serikali na watu binafsi huku akiwa na shauku ya kuiona nchi ya Tanzania inakuwa eneo zuri la uwekezaji kwa wenyeji na wageni wa mataifa mengine hali iliyompa umaarufu dunia kote na kufikia malengo ya Milenia ya Uchumi wa kati kwa Taifa hilo
WAKAZI WA MANISPAA YA KIGOMA/UJIJI NAMNA WATAKAVYOMKUMBUKA
Septemba 19, 2020 Rais Dr. John Pombe Magufuli alipokea ugeni wa Rais wa Burundi Mhe. Evaristi Ndayishimiye Manispaa ya Kigoma/Ujiji katika uwanja wa mpira wa Lake Tanganyika na kufungua jengo la Mahakamu Kuu ya Tanzania iliyopo katika Manispaa hiyo na kumbe bila kujua ilikuwa ziara yake ya mwisho hadi umauti unamkumba
Wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji watamkumbuka Rais Dr. Magufuli kwa miradi ambayo ameianzisha na kusimamia katika kipindi cha uongozi wake pindi alipokuwa hai
Ujenzi na Ukarabati wa Mwalo wa kibirizi ni mradi ambao umetekelezwa katika kipindi cha Hayati Dr. John Pombe Magufuli ambapo jumla ya fedha za Kitanzania Million 447,292,077/= zilitumika katika ukarabati wa mwalo huo ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa majengo ya usafirishaji wa mazao ya uvuvi nje ya Nchi na majengo ya kuuzia samaki na dagaa kwa wajasiliamali wadogo,
Pia ujenzi wa machinjio ujiji na kuwa ya kisasa unaendelea ambapo machinjio hayo yatasaidia kuongeza ubora wa nyama na kuhakikisha inafika kwa mlaji ikiwa salama na kufungua biashara ya nyama kwa Nchi jirani ambapo jumla ya fedha za Kitanzania Million 250,000,000/= zinatarajia kutumika huku tayari Serikali chini ya Hayati Rais Magufuli imeshatoa kiasi cha fedha za Kitanzania Million 184,000,000/= na ujenzi umeshaanza
Katika utekelezaji wa mradi wa Maji serikali ya awamu ya Tano ilitoa fedha za Kitanzania Million 42,000,000/= kwa ajili ya usambazaji wa maji kwa wananchi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma ukitarajia kuzalisha lita Million 142 kwa siku na mahitaji yakiwa lita Million 123 hadi kukamilika, kwa sasa mradi huo unasambaza maji lita Million 17 kwa siku, kwa wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na Mahitaji kwa sasa yakiwa ni lita Million 23 kwa siku hali ambayo imeleta matumaini makubwa kwa wakazi hao
Aidha Serikali ya awamu ya Tano chini ya Hayati Rais Dr.John Pombe Magufuli ilitekeleza ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma na ujenzi wa nyumba za Majaji kwa mwaka 2018/2019 ambapo kiasi cha fedha za Kitanzania Billion 8,900,649,022/= zilitumika katika ujenzi huo ambapo kukamilika kwa Mahakama hiyo kumeongeza uwajibikaji kwa watumishi na wananchi kupata haki zao kwa wakati ukilinganisha awali walivyokuwa wakisafiri hadi mkoani Tabora
Vituo vya afya vimeongezewa ufanisi katika utendaji kazi ambapo kituo cha afya cha Gungu na Ujiji vinatoa huduma ya upasuaji huku kituo cha afya cha Gungu jengo la upasuaji na kujifunguliwa kwa wanawake limejengwa amabapo serikali kuu ilitoa kiasi cha fedha Million 200,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo huku kaya za Manispaa hiyo 2400 walihamasishwa na kupata bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa
Wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji hakika wataendelea kumkumbuka Hayati Rais Dr. John Pombe Magufuli katika maeneo mbalimbali ambapo fedha za utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa na miundombinu ya shule kwa elimu Msingi kiasi cha fedha Billion 2,877,671,370/= zilitumika na elimu sekondari kiasi cha fedha Million 250,959,030/= zikitumika katika ujenzi, zaidi ya madarasa 86 yamejengwa, matundu ya vyoo 125, ukamilishaji wa maabara 11, ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu
Akifungua Bunge la 12 jijini dodoma wakati akihutubia Rais Dr. John Pombe Magufuli alitaja zao la Michikichi kuwa zao la kimkakati ambapo hadi sasa Halmashauri zote mkoani kigoma na taasisi mbalimbali zinazalisha miche ya kisasa ya michichikichi na kuigawa kwa wananchi bure ambapo zaidi ya miche 45,000 zimeshazalishwa manispaa ya Kigoma/ujiji na kuigawa kwa wakulima na wakazi wa Manispaa hiyo bure
Hakika ni Majonzi na simanzi ambayo Rais Dr. Magufuli ameyaacha ambapo itakumbukwa katika ziara yake ya mwisho Mkoani Kigoma alisema Serikali inampango wa kujenga meli mpya mbili zitakazotumika katika ziwa Tanganyika na zikiwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya mia sita na mizigo kila moja huku ujenzi huo utaenda sambamba na ukarabati wa meli zingine mbili ikiwemo Mv Liemba ambapo kiongozi huyo amefariki kabla ya kufikia lengo hilo huku wakazi wa Manispaa hiyo wakiwa na imani na Rais aliyepo sasa Mhe. Samia Suluhu Hassan kuendeleza miradi hiyo
Rais Dr. John Pombe Magufuli atakumbukwa na wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na itakuwa historia hata kwa vizazi vijavyo ikiwa ni pamoja na ujenzi na upanuzi wa uwanja wa ndege unaoendelea, ujenzi unaoendelea wa Bandari ya Nchi kavu Katosho, ujenzi wa bandari ya Ujiji na Kibirizi unaoendelea
Katika ziara iliyofanyika Nchini kwa baadhi ya mikoa ya Kuaga mwili na kutoa heshima za mwisho kwa Rais Dr. Magufuli Simanzi zimetawala kwa Watanzania walio wengi kuondokewa na mpendwa wao huku baadhi ya watu wakipoteza fahamu kutokana na Mapenzi waliyokuwa nayo na Rais huyo wengine wakimuaga kwa kutandika mavazi na Maua kama ishara ya heshima na kumuaga, lakini ni faraja kwa wakazi wa manispaa ya Kigoma/Ujiji wakiwa tayari kutoa ushirikiano kwa Rais mpya Mhe. Samia Suluhu Hassani baada ya kuapishwa katika kutekeleza na kuiendeleza miradi mbalimbali iliyopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Halmashauri zingine zote Nchini na Tanzania kwa Ujumla
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa