Na mwandishi wetu
Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana Novemba 28, wameahidi kufuta hati chafu katika kipindi watakachoitawala Manispaa ya Kigoma/Ujiji kutokana na ushirikiano watakaoufanya kati ya viongozi wa serikali za mitaa na wataalamu wa halmashauri hiyo
Aliyasema hayo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Kigoma Ndugu. Yassin Mtalikwa katika ukumbi wa manispaa hiyo katika sherehe za kuwaapisha wenyeviti wa mtaa na wajumbe waliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 24 Nchini wa kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa
Akihutubia wenyeviti, wajumbe wawilishi wanawake, wajumbe mchanganyiko, na waalikwa kiongozi huyo wa chama aliwataka viongozi hao waliochaguliwa kuwatumikia wananchi kwa kutatua matatizo yaliyopo katika ngazi ya mtaa
Aliendelea kuwataka viongozi hao waliochaguliwa kufanya kazi kwa ushirikiano baina ya Chama Cha Mapinduzi, na Serikali chini ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa kutambua matatizo yaliyopo ngazi ya mtaa si ya Mwenyekiti tu wa mtaa bali ni ya wadau wote wa maendeleo
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa wilaya hiyo Ndugu.Kitundu alisema Manispaa ya Kigoma/Ujiji sasa inaenda kupata maendeleo kutokana na wananchi kukiamini chama hicho na kukipatia ushindi utakaofanya viongozi hao kufanya kazi kwa ushirikiano ukilinganisha na uongozi uliopita kuwa uongozi Mseto
Aliwataka viongozi hao waliowachagua kufanya kazi kwa weledi na kuahidi kwamba viongozi hao watakuwa chachu ya maendeleo na watakuwa mfano wa kuigwa kutokana na mafunzo waliyoyopata ya kiuongozi na kuahidi barua zote za kuwapitishia wananchi zitakazopita kwa viongozi hao itakuwa zikitolewa bure
Alihitimisha kwa kusema ushindi kwa Chama Cha Mapinduzi ni hatua ya awali ya kuelekea uchaguzi mkuu kwa mwaka 2020 na kusema tayari wakazi wa Manispaa hiyo wamekielewa chama hicho na kuahidi kupata ushindi katika uchaguzi ujao
Naye mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndugu. Mwailwa Pangani aliwapongeza viongozi na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwa kupata ushindi wa 100% katika uchaguzi ulifanyika na kuwataka viongozi waliochaguliwa kuipatia ushirikiano katika kuhakikisha mapato ya halmashauri hiyo yanakuwa makubwa
“naomba ushirikiano wenu, na naamini kuchaguliwa kwenu itakuwa ni tiba kwa halmashauri kutokana na viongozi wote kuwa wa chama kimoja hivyo naamini mapato yatakuwa makubwa kutokana na ushirikiano mtakaouonesha ukilinganisha na uongozi uliopita” alisema Mkurugenzi huyo
Aliendelea kuwataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia usafi wa maeneo yao ya kiutawala wakishirikiana na watendaji wa mitaa na kata ili kuhakikisha manispaa hiyo inakuwa safi na mfano mzuri katika kujali afya za wakazi wa manispaa kutokana na ufunguzi wa dampo la kisasa uliofanyika hivi karibuni
Naye mmoja wa wenyeviti kutoka mtaa wa Mwanga Sokoni Mhe. Elia Mfaume aliwataka viongozi kwenda kufanya kazi kwa kutatua changamoto za wananchi na kuahidi kutoa ushirikiano kwa serikali na Chama Cha Mapinduzi
Sherehe hiyo ilihitimishwa kwa kuwaapisha wenyeviti 68 na wajumbe wawikilishi wanawake 136, na wajumbe mchanganyiko 204 kwa kuapa kiapo cha uadilifu, na kiapo cha utii na uadilifu wakiapishwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanzo Kigoma Bi. Mushi(kwa jina moja)
Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ni moja ya halmashauri iliyofanya uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, Chama Cha Mapinduzi kikiibuka kwa ushindi wa asilimia mia moja ambapo uchaguzi ulifanyika kwa kata 9 na kupata wenyeviti 14 na wajumbe 45 ambapo kata 10 tayari Chama Cha Mapinduzi kilikuwa kimeshapita bila Kupingwa
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa