Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji jana june 15, imepokea ugeni wa viongozi wa kisiasa kutoka nchini Burundi ikiwa ni kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa Jumuia ya Afrika Mashariki na kujifunza namna halmashauri inavyowahudumia wananchi kupitia miundombinu iliyoijenga.
Ugeni huo uliofika jana kutoka katika mji wa Nyanza Lake nchini Burundi ukiwa na Wabunge wawili(02), Mkuu wa Wilaya, Madiwani 19 pamoja na baadhi ya wataalamu wa mambo ya fedha ikiwa ni ziara ya siku mbili (02) katika halmashauri hiyo.
Akiwakaribisha wageni hao katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji Meya wa halmashauri hiyo Mhe. Hussein Ruhava aliwashukuru kwa kuchagua kuja kujifunza katika halmashauri hiyo kutokana na Nchi ya Tanzania kuwa na halmashauri nyingi.
Meya huyo Alisema “viongozi ninyi mliokuja ni viongozi wa kisiasa wenye dhamira ya kuwahudumia wananchi , kutimiza dhamira ya wananchi na kutekeleza huduma za jamii katika mahitaji ya wananchi jambo ambalo pia ni dhamira ya viongozi wa halmashauri yetu”.
Aliendelea kusema katika ziara hiyo waliyoichagua katika halmashauri hiyo wataweza kujifunza mambo mengi zaidi katika miradi watakayotembelea ikiwa baadhi ya miradi ni Nguvu ya wananchi na Miradi mingine ni kutoka serikali kuu.
Naye Barozi msaidizi katika ubarozi mdogo Mkoani Kigoma Mhe. Kabura aliweza kushukuru kwa mapokezi yaliyofanyika kwa viongozi kutoka nchini Burundi na kusema anaamini ziara itakuwa na tija kwa viongozi hao pamoja na wananchi wanaowaongoza katika maeneo yao ya kazi.
Baada ya ukaribisho huo katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ziara ilianza kwa kutembelea miradi mbalimbali pamoja na uwekezaji uliofanyika katika halmashauri hiyo ambapo jumla ya miradi 6 ilitembelewa na viongozi hao kutoka Nchi jirani ya Burundi ikiwa ni pamoja na Bandari ya Mkoa , Majengo ya madarasa mapya shule ya Msingi Kigoma, Mwalo wa Kibirizi, Stendi mpya ya Masanga, Soko la jioni Mwanga na forodha ya Ujiji.
Wakipewa taarifa katika Bandari ya Mkoa wa Kigoma namna inavyofanya kazi na Kaimu meneja wa bandari hiyo Ndugu. Madiwa Muhajiri alisema “ kwa sasa bandari inafanya kazi nzuri na inajiendesha kwa faida katika kipindi hiki cha awamu ya tano”.
Aliendelea kusema katika bandari hiyo wanasafirisha na kupokea mizigo kutoka katika nchi ya Burundi na nchi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na wanaeneo kubwa la kupakia na kushusha Mizigo, wana stoo ya kutunzia mali za wateja na usalama wa kutosha katika mizigo inayoingia na kutoka.
Aliendelea kusema kwa sasa hakuna udanganyifu wowote unaofanyika kutokana na vifaa vya kazi vilivyopo kama vile Mzani na bandari inajikita kutengeneza meli mpya kupitia shirika la meli( merine service)
Naye kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Frednand Filimbi akitoa taarifa katika soko la jioni la Mwanga (Mwanga night market) alisema soko hilo limejengwa kupitia wafadhili wa Local Investimate Climate (LIC) wanaojishughulisha katika kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na soko hilo linaleta matokeo mazuri katika kuwahudumia wakazi wa manispaa .
Nao baadhi ya viongozi kutoka katika mji wa Nyanza Lake nchini Burundi waliweza kuzungumzia ziara yao akiwemo Bi. Herena Senga mtaalamu wa masuala ya Fedha na Uchumi alisema “tumekuja ili tuone namna halmashauri hii ya manispaa ya Kigoma/Ujiji inavyowahudumia wananchi na mna rasilimali za kutosha naona ninyi mko matajiri sana ukilinganisha na tarafa yetu ya Makamba”.
Naye Naibu meya wa manispaa ya Kigoma/Ujiji akizungumzia ujio wa viongozi hao alisema “nimefurahishwa na ujio wa Viongozi hao na nimejifunza suala la upendo kwa viongozi hao waliokuja Nchini na ziara yao imekuwa fundisho hata kwa madiwani wa halmashauri yetu”
Katika ziara iliyoanza jana june 15 ikiwa ni ziara ya siku mbili katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma/Ujiji viongozi Wabunge hao, Mkuu wa wilaya na Madiwani wa mji wa Nyanza Lake watabadilishana na uzoefu wa kazi na namna wanavyowahudumia wananchi na madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ikiwa ni katika kudumisha ujirani mwema na kudumisha Jumuia ya Afrika Mashariki.
PICHA ZAIDI INGIA KATIKA MAKTABA YA PICHA.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa