Mkuu wa mkoa wa kigoma Brigedia Mstaafu Emmanuel Maganga ameagiza kwa shule zote za msingi na sekondari zilizopo katika mkoa wa Kigoma wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanajenga mabwawa ya samaki kwa ajili ya kitoweo na kujifunza stadi ya maisha.
Ameyasema hayo jana katika kilele cha sikukuu ya wakulima nane nane kanda ya magharibi alipokuwa akihutubia wananchi katika kufunga maonesho hayo yaliyofanyika mkoani Tabora eneo la ipuli katika uwanja wa Fatuma Mwasa ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Akihutubia uwanjani hapo aliipongeza serikali ya awamu ya tano kwa jitihada inayofanya katika kuwahudumia wakulima na wafugaji kwa kumaliza migogoro baadhi ya maeneo nchini na kuendelea kutenga maeneo ili kuondoa migogoro ambayo yaweza kujitokeza.
Aliendelea kusema mkoa wa kigoma kwa mwaka 2016 ulikuwa mkoa wa mwisho kiuchumi kitaifa lakini hadi sasa mkoa umepanda juu kwa nafasi tano kuonesha uchumi wa mkoa wa Kigoma unakuwa kila siku huku akiwakaribisha wawekezaji kujitokeza kwa kiwango kikubwa kuja kuwekeza katika mkoa wa Tabora na kigoma .
Aliendelea kuzitaka halmashauri za kanda ya magharibi kuendelea kukuposha na kutoa elimu kwa makundi ya wanawake, walemavu na vijana kupitia maafisa maendeleo wa jamii waliopo katika halmashauri hizo na kutokaa katika ofisi zao huku makundi hayo yakikiosa elimu ya ujasiliamali.
Aliendelea kusema maafisa ugani bado hawajafanya sehemu yao yao ya kazi ya kuwaelimisha na kuwatembelea wakulima na wafugaji katika maeneo yao ya kazi huku akiwataka wananchi kuwakamata maafisa hao pindi wanapokuwa wanatembea mitaani ovyo na kutoa taarifa katika ofisi ya mkuu wa mkoa huyo
Aliendelea kuzitaka kila halmashauri kubaki na maofisa ugani wa tatu ofisini na wengine wote kusambazwa katika vijiji kwa ajili ya kufanya majukumu yao na kuhakikisha uchumi wa familia , mikoa na nchi unakuwa kwa kasi inayotakiwa.
Akiendelea kuhutubia uwanjani hapo aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa ulioko mbele yetu na wanawake, wanaume na vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali huku akisisitiza kuchagua viongozi makini watakaoleta tija na matokeo makubwa kiuchumi ndani ya jamii.
Aliendelea kuzitaka halmashauri za mkoa wa Kigoma kuhakikisha ifikapo mwezi Septemba zinajenga mabanda yao ya kudumu ya maonesho ya wakulima katika eneo hilo la Ipuli viwanja vya Fatuma Mwasa na kuacha tabia za kupewa mabanda na halmashauri za mkoa wa Tabora.
Katika kuhititimisha hotuba na Mkuu wa mkoa huyo wa Kigoma aliongeza siku nne za maonesho kwa wakulima na wafugaji kwa lengo la kuendelea kujifunza na kufanya biashara mbalimbali zinazoendelea kufanyika katika eneo hilo.
Naye mkuu wa mkoa wa Tabora Ndugu. Agrey Mwani alimpongeza mkuu wa mkoa huyo wa Kigoma kwa kukubali kuja kuwa mgeni rasmi wa maonesho hayo ya wakulima na kufurahia ukaguzi wa mabanda alioufanya mgeni rasmi huyo na kutoa zawadi kwa halmashauri zilizofanya vizuri .
Mkuu wa mkoa huyo wa Tabora aliendelea kusema serikali ya awamu ya tano inajali masilahi ya wakulima na wafugaji na tayari zimetengwa Bilion mia sita za kuwasambazia maji wananchi wa mkoa huo kutoka katika ziwa Victoria.
Mkuu wa mkoa huyo alisisitiza wananchi wa kanda ya magharibi kuendelea kulima mazao ya kimkakati michikichi, pamba na tumbaku na kusema serikali kupitia taasisi za benki zinawakopesha wananchi mitaji ili kuweza kukuza mazao hayo.
Maonesho hayo ya kanda ya magharibi yamenogeshwa kwa nyimbo, maagizo na ngumi za bondia katika kusheherekea sikukuu hiyo huku wajasiliamali wakiendelea kufanya biashara mbalimbali katika eneo hilo la Ipuli katika viwanja vya Fatuma Mwasa.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa