Na Mwandishi Wetu
Hali ya kujaa kwa maji na kuathiri Wananchi wanaoishi jirani na Bwawa la Katubuka limeibuka Leo katika Baraza la Madiwani la kupokea na kujadili taarifa za Kata Manispaa ya Kigoma/Ujiji lililoketi Leo April 24, 2025.
Suala hilo limejadiliwa mara baada ya Diwani wa Kata ya Katubuka Mhe. Moshi Mayengo kuwasilisha taarifa za Kata hiyo.
Akizungumza katika Mkutano huo Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. David Rwazo amesema elimu imeendelea kutolewa kwa Wakazi wa maeneo hayo kuhama ili kuepuka kadhia ya ongezeko la maji kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema Serikali ikishirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo wakiwemo UNICEF na IOM (UN-Migration) wameshatoa Mahitaji ya kibinadamu kwa Wananchi wa eneo hilo kama vile Mchele, maharage, Sukari, Sabuni, dagaa magodoro, Shuka, na neti huku akisema Halmashauri imeomba Serikali kupitia Mradi wa TACTICS unaoendelea, kujenga Km 4.36 hadi kwenye mtaro wa asili wa Mungonya unaoelekeza maji yake ziwani.
Amesema tayari Ofisi ya Mkurugenzi imetenga eneo la kuhifadhi watu (Rescue area) katika Kata ya Katubuka na kutenga Chumba cha darasa Shule ya Msingi Majengo ili kuwasaidia wanaokosa eneo la kujihifadhi.
Barabara zilizovamiwa na maji tayari zimefungwa, na kukatwa kwa umeme katika eneo hilo huku akisema elimu imetolewa kwa Kamati za Maafa ngazi ya mtaa namna ya kukabiliana na kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Akizungumza katika kikao hicho Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Mhe. Ngenda Kilumbe Ngenda amesema tayari Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wameshafika Manispaa ya Kigoma/Ujiji katika kuhakikisha Wananchi hao wanapata msaada wa kibinadamu mara baada ya kutoa hoja ya dharura kujadiliwa Bungeni na Serikali kutuma Wataalamu.
Zaidi bofya www.kigomaujijimc.go.tz
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa