Na mwandishi wetu
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Msitaafu Emmanuel Maganga jana februali 18, alizindua zoezi la upuliziaji Mvuke katika makazi ya watu ikiwa ni mbinu ya kupambana na malaria na kuhakikisha Ugonjwa huo unakwisha kwa wakazi wa mkoa huo
Uzinduzi huo ulifanyika katika Zahanati ya Rusimbi iliyopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji ukihusisha viongozi wa serikali, Wanasiasa, wataalamu wa Afya, Asasi za kiraia na wananchi ukiwa na kauli mbiu ya “Zero Malaria inaanzia mimi na wewe”
Akitoa taarifa ya utekelezaji na upambanaji dhidi ya Ugonjwa wa Malaria, Mganga mkuu wa Mkoa Dkt. Saimon Chacha alisema kiasi cha watu kuambukizwa Malaria kimepungua , ambapo kimkoa kwa mwaka 2018 wagonjwa wa nje waliotibiwa katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali (OPD) ni 28.9% walikutwa na malaria ukilinganisha na mwaka 2019 wagonjwa wa nje (OPD) 26.7% ndio waliogundulika kuwa na ugonjwa huo
Aidha aliendelea kusema vifo vitokanavyo na Ugonjwa wa Malaria vimepungua ambapo kwa mwaka 2017 waliofariki kwa ugonjwa wa Malaria ni watu 472 na waliofariki kwa mwaka 2019 wakiwa ni watu 196 huku akieleza mafanikio hayo ni serikali kuboresha huduma za afya na upatikanaji wa vifaa tiba katika maeneo ya kutolea huduma
Akiendelea kutoa takwimu alisema yamekuwepo mafanikio ya mahudhulio ya Kliniki ya Baba, Mama na Mtoto ambapo wajawazito hupima ugonjwa wa Malaria pindi wanapohudhulia katika vituo vya kupima afya zao na kwa mwaka 2019 asilimia 100 ya wajazito walipima Malaria na kugundulika wagonjwa kupungua kutoka 11.9% kwa mwaka 2018 na kufikia 11.6% kwa mwaka 2019
Alisema mafanikio hayo yote ya kupungua kwa kasi ya ugonjwa wa malaria ni huduma bora inayotolewa ikishirikiana na Asasi za kiraia zinazopambana na ugonjwa huo huku dawa zikiwa zinapatikana katika vituo vya huduma kama ALU na Quinine, upuliziaji wa mvuke wa viua vidudu na ugawaji wa vyandarau kwa wajawazito na wanafunzi
Aliendelea kusema ugawaji wa vyandarua kwa wajawazito umeongezeka ambapo kwa mwaka 2019 wanawake wajawazito 110,776 walipata vyandarua sawa na asilimia 93.6% ukilinganisha kwa mwaka 2018 ambapo wajawazito 826 walipata vyandarua sawa na ongezeko la 10.9%
Alisema shule za msingi 657 zikiwa na walengwa wanafunzi 29,684 kwa mkoa wa Kigoma waligawiwa vyandarua vyenye viatilifu vya mda mrefu, na kusema kwa mwaka 2019 mwezi julai mkoa ulipokea lita 7616 za viua dudu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto na kusema hadi kufikia mwezi Desemba tayari zaidi ya lita 2000 zimeshapuliziwa kwa njia ya mvuke katika makazi ya watu
Alihitimisha kwa kusema kampeni ya upuliziaji mvuke itakayozinduliwa na Mkuu wa Mkoa, upuliziaji huo utafanyika kwa Wilaya,Tarafa, Kata, Vijiji na Mitaa yote ya mkoa wa Kigoma na makazi ya watu wote huku akisema magari ya upuliziaji mvuke huo yatapita katika makazi ya watu na kuwataka wakazi kufungua milango na madirisha pindi gari hilo la mvuke litakapokuwa likipita katika mitaa na makazi ya wananchi
Naye Mkuu wa mkoa akihutubia katika mkutano huo alisema kwa mwaka 2018 mkoa ulikuwa katika orodha ya mikoa mitano (5) yenye idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Malaria na kusema idara ya afya inastahili kupongezwa kwa jitihada zilizofanyika kuhakikisha malaria inapungua
Alisema “kampeni ya leo ikawe ni vita kamili ya kupambana na Mbu wapevu na wadudu wengine wahalibifu na niwaase wananchi wote hakikisheni gari letu la mvuke litakapopita katika mitaa yenu madirisha na milango iwe wazi kwa ajili ya kuua wadudu hao na kuondokana na Ugonjwa huo na nawahakikishia Zero Malaria inawezekana”
Aliendelea kusisitiza kuwa mvuke huo hauna madhara yeyote , na kumuagiza mkuu wa wilaya hiyo kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakoa sambaza na kuzusha madhara yatokanayo na mvuke huo kutokana na tabia za baadhi ya wakazi wa Mkoa huo kuwa na utamaduni wa kuzusha maneno ya uongo
Alihitimisha wananchi kuwa tayari na kupambana na ugonjwa huo kutokana na ugonjwa huo kuwa na madhara ya kiuchumi na kusema ni rahisi kuzuia ugonjwa huo lakini pia ni gharama katika uponyaji na kuwahudumia wagonjwa
Naye mkuu wa wilaya Ndugu. Samsoni Anga alipongeza jitihada zinazofanywa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa kupitia idara ya Afya kuhakikisha Zero malaria inawezekana katika mkoa huku akiahidi kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale wote watakaobainika katika upotoshaji wa zoezi hilo la upuliziaji Mvuke
Naye Meya wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Mhe. Hussein Ruhava alipongeza jitihada za mkuu wa mkoa za kupambana na ugonjwa wa malaria huku akiahidi Manispaa chini ya madiwani kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa na kusema maendeleo hayana chama
Mkutano huo ulihitimishwa na Mkuu wa Mkoa kwa kuzindua mashine za upuliziaji mvuke.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa