Katibu mkuu wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Zainabu Chaula jana februali 10, amemtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji kutenga maeneo maalumu ya kuzika watu wanaokufa kutokana na magonjwa ya mlipuko
Katibu mkuu huyo ametoa tamko hilo ikiwa ni katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayoendelea kuathiri baadhi ya Nchi Duniani, ambapo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inameathiriwa na Ugonjwa wa Ebola huku Nchi ya China ikiendelea kuathiriwa na vifo kutokana na ugonjwa wa Corona
Katibu Mkuu alisema lengo la ziara yake ni kukagua namna huduma za afya zinavyotolewa kwa Wananchi na kuangalia namna Mkoa na Halmashauri zilivyojiandaa katika kukabiliana na wagonjwa wa magonjwa hayo yamlipuko kutokana na kuwa pembezoni na mipakani ya nchi jirani
Akiwa katika zahanati ya Bangwe ambapo ndipo kituo cha kuwahudumia wagonjwa wa Ebola na Corona endapo watabainika kuwepo, alisomewa taarifa ya Utendaji kazi wa Zahanati hiyo ambapo kwa mjibu ya Sensa ya Mwaka 2012 eneo hilo lina jumla ya wakazi elfu kumi na tisa (19,000) na Zahanati hiyo inapokea wagonjwa wa nje sitini (60) kwa siku , na kutoa huduma ya Kliniki ya baba, Mama , na watoto huku ikiwa na watumishi kumi na moja (11)
Katibu mkuu huyo aliendelea na ziara yake hadi katika Zahanati ya Kigoma ambapo alisomewa taarifa na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Ndugu. Godlove Myinga kuwa Zahanati hiyo inahudumia wakazi wa Kata ya Kigoma yenye wakazi 21577 kwa mjibu ya Sensa ya mwaka 2012 na kusema zahanati hiyo ina watumishi 22 ambapo inahudumia wagonjwa wan je elfu moja (1000)kwa mwezi, wastani wa wanawake 30 hujifungua kwa mwezi,huku huduma zingine za upimaji wa VVU hutolewa, upimaji wa saratani ya Shingo ya Kizazi na huduma ya uzazi wa mpango hutolewa
Mganga mfawidhi huyo aliendelea kueleza mafanikio ya zahanati ya Kigoma kuwa hadi hivi sasa imeweza kupanda kutoka nyota moja hadi kufikia nyota mbili, na kusema huduma ya wanawake ya kujifungua inatolewa huku akisema uboreshaji wa mazingira kwa kupanda miti na utengenezaji wa bustani unaendelea ili kuwa kivutio na faraja kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma
Alisema licha ya mafaniko hayo zipo changamoto ambazo zinapaswa kutatulia kwa zahanati hiyo kuwa na eneo dogo ukilinganisha na idadi kubwa ya wateja wanaofika kupata huduma huku akiomba kuongezewa kwa eneo lililokuwa ofisi ya Halmashauri ya Kigoma kabla ya kuhama ofisi hizo na kuomba majengo ya Sandra yanayomilikiwa na halmashauri ya Uvinza
Naye katibu mkuu amepongeza shughuli zinazofanywa na watumishi wa Zahanati zote mbili kwa kuwahudumia wananchi na wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji huku akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa
Alisema katika zahanati ya Bangwe huduma zinazotolewa ziendelee kutolewa kwa wagonjwa wa kawaida na endapo wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko watabainika(kugundulika) kuwepo kutokana na dalili za magonjwa ya Ebola na Corona huduma zitasitishwa kwa wagonjwa wakawaida na kuhamia zahanati ya Kigoma
“hadi hivi sasa hakuna mgonjwa aliyebainika kuwepo Nchini wa magonjwa haya ya Ebola na Corona inayoendelea kuwatesa wenzetu Wachina, tayari tumeshachukua tahadhari katika maeneo yetu ya Mipaka, Bandarini na Viwanja vya Ndege, wapo watu wanaendelea kuchunguza na wanavifaa maalumu kwa hiyo Watanzania wasiwe na wasiwasi waendelee kufanya kazi lakini pia lazima tuchukue tahadhari katika kuhakikisha magonjwa haya hayaingii nchini na endapo mgonjwa atabainika tujue namna ya kumhudumia na wapi huduma hizo zinaweza kutolewa” alisema katibu Mkuu huyo
Alihitimisha kwa kuwataka watumishi wa afya kufanya kazi kwa kujiwekea malengo ili kutoa huduma zilizo bora na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufatilia majengo hayo yanayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Uvinza kwa kufanya mazungumzo ili kupata Majengo hayo kwa lengo la zahanati hiyo kuipandisha hadhi kuwa kituo cha afya
Naye mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ndugu. Mwailwa Pangani alimpongeza Katibu mkuu huyo kwa kufanya ziara katika Manispaa hiyo na kuahidi kutenga eneo la makaburi la kuzika watu wanaofariki kwa magonjwa hatari na ya mlipuko huku akiahidi kufatilia majengo yanayomilikiwa na Halmashauri jirani katika Manispaa hiyo
.Maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, yalionekana kuongezeka mwaka jana 2019 Mashariki mwa Demokrasia ya Congo, baada ya kuzuka kwa ugonjwa huu hatari ambapo hadi hivi sasa inasemekana kasi ya maambukizi ya Ugonjwa huu umepungua nchini humo
Watu zaidi ya 1,800 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 2,000 kuambuakizwa virusi vya ugonjwa huo, kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO),
Wakati nchi ya China ikiendelea kupambana na ugonjwa wa Corona watalaamu walieleza watu zaidi ya 75,000 wanaweza kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, katika mji wa Wuhan, huku vifo hadi kufikia jana vikiwa vifo 908 vilivyotokana na ugonjwa huo kwa mjibu wa vyombo vya habari vya kimataifa
Picha na video zaidi ingia katika maktaba ya picha www.kigomaujijimc.go.tz
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa