Na Mwandishi Wetu
Mafunzo namna ya kujikinga na kukabiliana na Majanga mbalimbali yameendelea kutolewa kwa Wananchi wa Wilaya ya Uvinza kwa Kata za Ilagala, Sunuka, na Mwakizega.
Elimu hiyo imeendelea kutolewa Jana Oktoba 19, 2023 na Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu idara ya Menejimenti ya maafa katika Ofisi za Kata ya Ilagala kwa lengo la kuwawezesha Wananchi kukabiliana na kupunguza madhara yatokanayo na majanga.
Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Naibu Kamishina Hamisi Mrutengo akiwasilisha mada kwa wajumbe wa kamati za maafa ngazi za Kata aliwataka kuendelea kutoa elimu katika maeneo yao na kuweka mipango kazi ya kupunguza madhara yatokanayo na majanga ya asili.
Aidha katika mafunzo hayo mada za mfumo wa Usimamizi wa maafa na Tathimini za Maafa zimewasilishwa na Wataalamu hao pamoja na kujadiliwa.
Mratibu wa Maafa Mkoa wa Kigoma Ndugu. Msafiri Nzunuri amewashukuru Wataalamu Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa namna ambavyo wameendelea kuielimisha jamii huku akiwataka Wananchi kuanza kuchukua tahadhari mapema kutokana na mazingira hatarishi.
Mamlaka ya hali ya hewa Nchini Tanzania (TMA), Mwezi Julai ilitoa taarifa juu ya mwenendo wa hali ya El Niño katika bahari ya Pasifiki na athari zake.
El Niño ni mfumo wa hali ya hewa unaosababishwa na uwepo wa ongezeko la joto la juu ya wastani katika eneo la kati ya kitropiki la bahari ya Pasific. Hali hii huambatana na athari mbalimbali ikiwemo ongezeko la Mvua, Joto na Hali ya Ukame katika maeneo mbalimbali ya Dunia.
Nchini Tanzania hali ya El Niño huambatana na vipindi vya Mvua kubwa na za Juu ya Wastani.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa