Na Mwandishi wetu
Manispaa ya Kigoma/Ujiji leo march 5, 2021 imekabidhi vifaa vya Usafi vilivyogharimu kiasi cha fedha za Kitanzania Million themanini na tatu (83,000,000/=) kwa vikosi kazi vya Usafi ishirini na mbili (22) ili kuhakikisha mji unakuwa katika hali ya usafi
Vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa vikosi kazi vya usafi vya mitaa vilivyoundwa na wataalamu ngazi ya kata wakishirikiana na wenyeviti wa mitaa ili kuhakikisha mji unakuwa safi kupitia Usafi utakaofanyika na kuchangia tozo za uzoaji wa taka hizo
Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi, Mganga Mkuu wa Manispaa Dr. Sebastian Siwale amewataka watendaji kata na mitaa kuhakikisha wanasimamia vikosi kazi vya usafi katika mitaa yao ili kuhakikisha mji unakuwa safi wakati wowote
Aidha Mganga Mkuu huyo amevitaka vikosi kazi vya usafi kufanya kazi hiyo kwa uaminifu kwa kukusanya taka katika barabara za mji, Makazi na Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali kwa wakati ili kuepuka mrundikano wa uchafu unaoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kwa binadamu kutokana na kukabidhiwa kwa vifaa vitakavyorahisisha shughuli hiyo
Kaimu Mkuu wa idara ya Usafi na Mazingira Ndugu. Elishaphati Rusemvya amesema kwa sasa Manispaa ya Kigoma/Ujiji inazalisha tani mia moja hamsini na mbili (152)kwa siku ambapo taka hizo husafirishwa kwenda dampo la Kisasa lililopo Msimba linalomilikiwa na Manispaa hiyo
kiongozi huyo amewataka wakazi wa Manispaa kuachana na tabia ya kulima katika hifadhi za barabara na kuacha tabia za upandaji wa mazao marefu na kufanya hivo ni kinyume na sheria ndogo hali inayoweza kusababisha mwananchi kushitakiwa kwa kuvunja sheria hiyo, Aidha amehitimisha kwa kuzitaka Taasisi mbalimbali na wananchi kutoa ushirikiano kwa kufanya Usafi wa Mazingira na kuhakikisha taka hizo zinafikishwa katika vizimba vilivyowekwa mtaani kupitia vikosi kazi
Mtendaji wa Kata ya Kigoma Ndugu. Kasimu Nyamkunga amesema wao kama wataalamu watahakikisha wanasimamia vikosi kazi vya usafi ili kuhakikisha mji unakuwa safi katika mitaa mbalimbali na makazi ya watu
Katika shughuli zinazofanywa na vikosi hivyo ni pamoja na usafi wa barabara za mji, uzoaji taka kwa makazi na Taasisi ambapo kila kaya hulipia kiasi cha fedha za Kitanzania Tsh 1000/= na taasisi kuanzia elfu thelathini hadi laki mbili (30,000/= hadi 200,000/=) kwa mwezi kutokana na ukubwa wa Taasisi na uzalishaji taka
Vifaa hivyo vya Usafi vimekabidhiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kutokana na msaada uliotoka kwa kampuni ya Belgium Development Agency inayojishughulisha na uchakataji wa taka na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya , vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja na Troli kubwa 44, Troli ndogo 44, Mifagio 220, reki 220, rain boot(Gambuti) 220, gloves 220, na Koreo 220
Kampuni hiyo inayojishughulisha na uchakataji wa taka Makao Makuu yao yapo Mji Mkuu wa Bunjumbura Nchini Burundi ikiwa inafanya kazi Nchi tano (05) za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia , Burundi na Rwanda
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa