Halmashauri ya manispaa ya Kigoma/Ujiji leo October 10, imefanya ziara katika eneo la Katosho kata ya Gungu na uongozi wa Shirika la reli Tanzania(TRC) katika kutatua mgogoro wa kuvunja makazi ya wananchi wa eneo hilo kwa madai kuwa ni eneo la shirika hilo.
Ziara hiyo imefanyika katika eneo hilo ikiwa ni sera ya serikali ya awamu tano wananchi kutosumbuliwa katika makazi yao kama watakuwa hawaja vunja sheria za nchi ambapo eneo hilo lina zaidi ya nyumba za makazi 25 na viwaja vya wananchi 12.
Katika ziara hiyo wataalamu, madiwani wa manispaa hiyo pamoja na wataalamu wa shirika la reli (TRC) wameweza kujilizisha kwa kuchukua vipimo vya eneo la shirika la reli ambapo imebainika kuwa awali eneo la katosho ndio ilikuwa eneo la kituo cha treni(Stesheni) ambapo vipimo vinakuwa tofauti na eneo la njia ya reli ya kawaida kuwa na vipimo vya mita 30 kutoka katika njia hiyo kwa pande zote mbili.
Katika eneo hilo lililopimwa vipimo vilivyochukuliwa ni mita 90, mita 112, mita 156 kutoka usawa wa eneo la reli ambapo baadhi ya nyumba zimeonekana kuwa katika eneo la vipimo hivyo licha ya sheria ya awali ya shirika hilo kuwa mita 30 kutoka reline kwa pande zote mbili
Akiongea katika ziara hiyo Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Mwailwa Pangani amesema shirika la reli linalo wajibu wa kuomba ardhi kwa halmashauri kama shirika hilo litakuwa na uhitaji jambo ambalo halmashauri haikuwahi kupokea maombi hayo na shirika la reli kutoweka mipaka ya eneo linalodaiwa kuwa la shirika hilo .
Ameendelea kusema eneo hilo linalodaiwa na shirika la reli limepimwa na halmashauri mwaka 2002 na kugawiwa kwa wananchi, ambapo ni miaka zaidi ya kumi na mbili (12) wananchi wakiishi katika eneo hilo na kisheria makazi hayo ni halali kwa wakazi wa eneo hilo.
Naye Afisa wa ardhi wa shirika la reli(TRC) Ndugu. Fredrick Kusekwa amesema maeneo yanayomilikiwa na shirika hilo yanawekewa alama na yanalindwa na kuna makazi yamewekwa kando ya reli na yanayokaliwa na wataalamu wa shirika hilo kwa lengo la kulinda maeneo hayo ambapo amesema katika kushughulikia mgogoro huo wa ardhi ni muhimu taasisi hizo kukaa pamoja katika mazungumzo ambayo hayatoathiri upande wowote wa taasisi na athari kwa wananchi.
Naye afisa wa dawati la malalamiko manispaa ya Kigoma ujiji Ndugu. Melleji Mollel amesema halmashauri imekuwa ikitatua malalamiko ya wananchi na mgogoro huo wa wakazi wa eneo hilo la katosho kando ya reli hatimaye unaelekea kupata suluhu kutokana na taasisi hizo mbili kuwa na lengo moja la kutowaathiri na kuwasumbua wakazi wa maeneo hayo.
Naye katibu wa wahanga hao wa eneo la katosho Bi. Emelda Albeto ameipongeza halmashauri ya manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa jitihada na ukaribu ambao wamekuwa wakiuonesha kwa wahanga hao na kusema ujio wa viongozi kutoka shirika la Reli inaonesha ni namna gani tatizo hilo linaenda kuisha na wanaamini taasisi hizo zitazingatia maslahi ya wananchi hao.
Akihitimisha katika ziara hiyo iliyofanyika naibu meya wa halmashauri hiyo Mhe. Athumani Athuman amesema taasisi hizo mbili zitakaa pamoja na andiko litakwenda kwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la reli(TRC) la kuwataka wakazi hao kutovunjiwa na endapo shirika litahitaji matumizi ya eneo hilo iweze kuwalipa wananchi wa eneo hilo.
picha zaidi ingia katika maktaba ya picha
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa