Na mwandishi wetu
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali katika Sekta ya Afya na Elimu Mkoani Kigoma ambapo jumla ya fedha za Kitanzania Shilingi billion kumi na tano million mia nane themanini ( 15,880,000,000/=) zimetengwa katika ujenzi wa Miradi hiyo
Manispaa ya Kigoma/Ujiji tayari imepokea fedha za Kitanzania Shilingi million mia tisa sitini (960,000,000/=) ikiwa ni fedha kutoka Serikali Kuu na ni mpango wa Rais wa Tanzania kuinua Uchumi wa Watanzania kutokana na athari za Uviko-19 zilizojitokeza duniani kote
Kiasi cha fedha hicho kinatarajia kutumika katika Ujenzi wa Madarasa arobaini na nane (48) kwa shule kumi na sita (16) za sekondari zilizopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambapo jamii itahusika katika ujenzi wa madarasa hayo
Fedha hizo zilizotolewa zinatarajia kuleta manufaa kwa Wananchi na Wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambapo miongoni mwa faida zinazotarajia kupatikana ni pamoja na;-
Ajira kwa Wananchi na wakazi wa Manispaa ya Kigoma, zaidi ya ajira mia tisa sitini (960) zinatarajiwa kuzalishwa katika kipindi chote cha ujenzi wa madarasa utakapokuwa ukiendelea ambapo kwa kila darasa linatarajia kugharimu kiasi fedha Million ishirini (20,000,000/=) na kuzalisha ajira ya watu Kumi na tano hadi ishirini(15-20)
Kuongezeka kwa mzunguko wa fedha, ununuaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali kama vile ununuzi wa mawe, Mchanga, kokoto, cementi, mbao, mabati, na vifaa vingine vya ujenzi unatarajia kuongezeka kutokana na kuhitajika katika ujenzi huo ikiwa ni pamoja na upakiaji, upakuaji na usafirishaji wa vifaa hivyo na kufanya uwepo wa mzunguko wa fedha kwa haraka
Kukua kwa Uchumi wa Wananchi na Wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, katika kipindi chote cha ujenzi ajira mbalimbali zitazalishwa ambapo idadi kubwa itakuwa ikijishughulisha kufanya kazi ambapo makundi mbalimbali kama vile, mafundi uashi, Ujenzi, Vibarua na mama/Baba lishe watajiongezea kipato na kufanya uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na hata jamii kukua
Kuboreshwa kwa miundombinu ya Kujifunzia na Kujifunzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akizungumzia usimamizi wa fedha hizo aliwataka wataalamu kusimamia miundombinu ya ujenzi katika viwango vinavyofaa ambapo alitamka kuwa hatakuwa na huruma kwa mtu atakaye tumia fedha hizo kwa kujenga katika viwango vya chini , hivyo tunatarajia miundombinu itakayokuwa katika viwango vinavyokubalika na kuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi na walimu katika tendo la ufundishaji na Ujifunzaji
Idadi kubwa ya wanafunzi kupata nafasi ya Kujiunga na elimu ya upili, kumekuwa na ongezeko la ukuaji wa ufaulu kwa mitihani ya mwisho kwa wanafunzi wa darasa la saba kutoka ufaulu wa asilimia themanini (80%) kwa mwaka 2016 hadi ufaulu wa asilimia themanini na sita (86%) kwa mwaka 2021 hivyo ujenzi wa miundombinu hiyo itakuwa chachu ya idadi kubwa ya wanafunzi kujiunga na elimu ya upili kutokana na uwepo wa miundombinu bora
Kiwango cha elimu na ufaulu kwa wanafunzi wa shule za Upili kuongezeka, katika madarasa yatakayojengwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji wanafunzi watakuwa wakijifunza katika mazingira bora kwa kiwango kinachofaa kama vile ukaaji darasani hivyo kufanya wanafunzi kujifunza katika mazingira yatakayofanya kupata kiwango kikubwa cha elimu na kuleta matokeo chanya kwa jamii na hata kukua kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao
Kuwa na jamii kubwa iliyoelimika, kukamilika kwa ujenzi ya madarasa hayo kutafanya idadi kubwa ya wanafunzi wa wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kujiunga na masomo ya upili na kuwa na idadi kubwa ya watu walioelimika na elimu hiyo kuitumia katika maisha ya kila siku na kufanya kuwa na jamii iliyoendelea katika nyanja mbalimbali
Madarasa hayo yanatarajia kujengwa kwa shule za Sekondari Buteko, Kitwe, Buhanda, Buzebazeba, Gungu, Buronge, Bushabani, Kigoma-Ujiji,Kitongoni, Kichakachui, Kirugu, Katubuka, Masanga, Mwananchi, Rubuga, na Shule ya sekondari Rusimbi
Taarifa zaidi endelea kufuatilia taarifa zetu kupitia www.kigomaujijimc.go.tz
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa