Na mwandishi wetu
Jana February 25, 2021 Mkutano wa Baraza la Madiwani (Full Council) la kupokea taarifa za kata lilijadili changamoto ya ukosefu wa zahanati Mtaa wa Mgumile kata ya Kagera kutokana na eneo lililokuwa linajengwa awali kujaa maji na kusababisha miundombinu kuharibika na kusitishwa kwa ujenzi huo
Awali Diwani wa Kata hiyo Mhe. Gregory Keberezo Akiwasilisha taarifa ya robo ya pili kwa kipindi mwezi Oktoba hadi Desemba 2020/2021 alisema kwa mjibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 idadi ya watu mtaa wa Mgumile ilikuwa ni Wanawake 1319, wanaume 1476 na kufanya jumla ya watu kuwa 2795, na kaya zikiwa 633 huku akisema idadi hiyo imekuwa ikiongezeka
Diwani huyo aliendelea kusema kutokana na changamoto iliyojitokeza ya kujaa kwa maji ya ziwa eneo ambalo awali zahanati hiyo ilikuwa inaendelea kujengwa anatarajia kufanya mkutano na wananchi wiki ijayo ili kujadili namna ya kufanikisha kupata eneo jingine la kujenga zahati hiyo
Naye mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Mwailwa Pangani akizungumzia mpango wa ujenzi wa zahanati katika mtaa huo alisema kwa sasa tayari fedha kutoka Serikali kuu imeleta fedha kiasi cha Millioni Hamsini (Tsh 50,000,000/)= kwa ajili ya kuendeleza ujenzi katika mtaa huo huku akisema kutokana na kujaa kwa maji katika eneo la awali pindi wananchi watakapo pata ardhi kutokana na jitihada ambazo tayari wameanza kuzionesha ujenzi huo utaanza haraka
Mwenyekiti wa baraza hilo na Meya wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Mhe. Baraka Lupoli alimtaka diwani wa Kata ya Kagera kusimamia na kufanya mkutano kwa wakati juu ya upatikanaji wa eneo hilo kwa wananchi na ujenzi kuanza haraka kutokana na uwepo wa fedha na wananchi kutoendelea kupata taabu ya kupata matibabu
Naye Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Mhe. Ng’enda Kirumbe aliipongeza Serikali kwa kiasi cha fedha kilicholetwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo huku akisema yeye kama Mbunge wa eneo hilo ataendelea kuisemea zahanati hiyo ya Mgumile na huduma zote za afya katika Jimbo lake hilo na kuendelea kutafuta fedha kwa wadau mbalimbali ili kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo ili kufikisha huduma za jamii kwa karibu kwa wananchi na wakazi wa eneo hilo
Mtaa wa Mgumile ni moja ya mitaa minne(04) ya kata ya Kagera inayopatikana Manispaa ya Kigoma/Ujiji Tarafa ya Kigoma Kusini ambapo mtaa huo upo nje kidogo ya Mji kando mwa ziwa Tanganyika na wananchi wake wakijishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara hasa zao la Michikichi katika Bonde la Mto Ruiche na ujenzi wa shule ya mda wa shule ya Msingi Mgumile imejengwa eneo jingine kutokana na kuvamiwa na maji hayo ya ziwa
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa