Waziri mkuu wa Tanzania Mhe. Kasimu Majaliwa atoa mwezi mmoja kwa baraza la madiwani kujirekebisha kutokana na migogoro inayoendelea baina ya madiwani na wataalamu(ofsi ya mkurugenzi) katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji.
Ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kawawa jana jumamosi july 28, uliopo eneo la Ujiji, ambapo amesema halmashauri iko katika hali ambayo sio nzuri kwani ina hati chafu tatu mfululizo , migogoro nayo ya madiwani na wataalamu, ameahidi kulivunja baraza hilo kama madiwani watashindwa kujirekebisha ndani ya mwezi mmoja ,“kauli yangu ni ya mwisho tutavunja baraza la madiwani” alisema waziri mkuu .
Licha ya kuahidi kulivunja baraza hilo la madiwani alimsifia mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Dr. John Shauri Tlatlaa kwa kazi anayoifanya alisema “mkurugenzi endelea kufanya kazi, tumekaimisha mkurugenzi kwa majaribio”.
Waziri mkuu huyo katika ziara yake iliyoanza asubuhi baada ya kushuka uwanja wa ndege uliopo halmashauri ya Kigoma Ujiji aliweza kwenda Ikulu kwa ajili ya kusaini kitabu cha wageni ambapo aliambatana na waziri wa elimu Mhe. Joyce Ndalichako, naibu waziri wa kilimo mhe. Omary Nkumbo, naibu waziri wa nishati na madini, naibu waziri wa mawasiliano, wabunge wa halmashauri za kigoma, akiwa katika ukumbi wa ikulu na mkuu wa mkoa Ndugu Emmanuel Maganga, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri , wenyeviti wa halmashauri na kuwajulisha lengo la ziara yake ni kuzindua siku ya michikichi kwa mkoa wa Kigoma na halmashauri zote zinazolima zao la michikichi nchini.
Baada ya kikao Ikulu waziri mkuu huyo alielekea katika mkutano uliofanyika ukumbi wa jengo la NSSF liliopo katika manispaa ya kigoma ujiji kukutana na wadau wa michikichi wakiwemo wakulima, wakamua mawese, wafanyabiashara , taasisi za utafiti katika zao la michikichi, mabenki na watumishi wa halmashauri hiyo.
akiwa katika ukumbi huo alianza kwa kusema “naanza ziara yangu mkoani kigoma kwa halmashauri zote isipokuwa halmashauri ya Kakonko na Kibondo kwa lengo la kuhamasisha michikichi” aliendelea kusema “Kigoma ndioinazalisha zaidi mafuta ya mawese nchini , Malaysia iliyoendelea kwa sasa kwa zao hilo mbegu waliitoa mkoani hapa katika kijiji cha Simbo na leo wanatuzidi sasa, hatuwezi kukubali”.
Aliendelea kuwataka watumishi waliopo mkoani Kigoma kwa sasa kubadilika na kuwa na mawazo chanya yatakayoleta tija kwa zao hilo na ukuaji mkubwa wa uchumi kwa mkoa hata kwa Taifa, aliwajulisha wadau hao kuwa maamuzi ya mkutano hayo yatakayotolewa kila mmoja kwa nafasi yake aweze kuyasimamia na kuyafanyia kazi.
Aliwataka wadau wote waliohudhulia kutoa mwelekeo wa kuendeleza zao hilo la michikichi ambapo kampuni ya Trade Mark ya Afrika Mashariki waliweza kutoa Dolla million tano kupitia kwa mkurugenzi wa kampuni hiyo Ndugu. John(kwa jina moja) kwa lengo la kuendeleza zao hilo na kuzalisha mbegu ili wananchi waweze kupata mbegu bure, lakini pia wadau wa benki waliweza kujitokeza wakiwemo benki ya kilimo Tanzania(TAB), benki ya maendeleo(TDB) , ambapo mkurugenzi wa benki hizo zikiungana kwa lengo la kuendeleza zao hilo la michikichi Ndugu. Japheti Jastini aliwataka wakulima na kuwajulisha mikopo iko wazi kwa wakulima na wakamuaji mafuta ambapo waliwataka wakulima hao kujitokeza huku wakisema ofsi zao kwa sasa zitakuwa katika benki ya posta lakini pia benki ya CRDB nao kupitia mkurugenzi wake Ndugu Joel Mwageni waliweza kuwakaribisha wakopeshaji na wajasiliamali wanaotaka kuendeleza zao hilo la michikichi.
Mmoja wa wakamuaji wa ngazi zao litokanalo na michikichi kwa lengo la kupata mafuta aliweza kueleza changamoto wanazozipata katika teknolojia kwa kusema mashine wanazozitumia ni za zamani ambapo ni mashine zinahitaji maji ya moto ambapo maji ya baridi inaathiri mashine hizo na kufanya mafuta mengi kutomalizika wakati wa ukamuaji ambapo alimpongeza waziri mkuu kuonesha jitihada za kufanikisha katika suala la teknolojia.
Nao wakulima wakiwakilishwa na Moshi Rashidi waliweza kueleza changamoto wanazozipata katika bonde la mto Luiche, ambapo wakati wa kiangazi hutokea ukame na katika kipindi cha mvua hutokea mafuriko na kufanya mazao kuzama, ambapo waziri mkuu Mhe. Kasimu Majaliwa aliweza kuwataka wataalamu kuja na mbinu ya kutatua changamoto hiyo kwa kutengeneza mifereji hiyo kipindi cha mvua kuvuna maji na kuyaweka sehemu moja na kuyarudisha mashambani kiangazi pindi maji hayo yanapohitajika mashambani.
MAAGIZO KWA WADAU WOTE WA ZAO LA MICHIKICHI
Katika mkutano huo uliochukua takribani ya masaa matatu waziri mkuu aliweza kutoa maagizo zaidi ya kumi kwa lengo la kufanikisha zao hilo na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na hata Taifa kwa ujumla. Maagizo hayo ni
Kila mkoa na halmashauri zote nchini zinazolima zao la michikichi kuanza kuweka mikakati ya kuendeleza zao hilo la michikichi.
Wakurugenzi wote nchini kuweza kuanza kuratibu namna ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo la michikichi.
Halmashauri kuanza kuhamasisha upandaji wa michikichi majumbani , maeneo ya burudani na katika kumbi za starehe,kando kando ya barabara na mashambani.
Taasisi zote nchini shule, magereza , na JKT kuanzisha mashamba ya michikichi.
Kila halmashauri mkoani Kigoma ianzishe kitalu cha miche million moja na December 30 atarudi mkoani kwa lengo la kukagua vitalu hivyo.
Halmashauri zote nchini waweze kutambua taasisi binafsi na mashirika yanayojihusisha na zao la michikichi.
Waziri mkuu huyo alimamaliza kwa kuwashukuru wadau wote waliohudhulia mkutano huo na kusema chuo cha maendeleo ya jamii Kihinga kwa sasa kitakuwa kituo cha utafiti wa mbegu za michikichi ili kuweza kuleta ufanisi wa zao hilo kwa mkoa wa Kigoma.
Waziri mkuu huyo yupo mkoani kigoma hadi july 31 kwa kutembelea halmashauri zote kwa lengo la kukuza zao la michikichi ambapo atatembelea halmashauri zote isipokuwa kakonko na kibondo kwa lengo la kupisha shuguli za uchaguzi zinazoendelea.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa