Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa wilaya ya Kigoma Bi. Ester Alexander Mahawe leo October 8, 2021, amefanya kikao na Viongozi wa Machinga waliopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa lengo la kujadiliana maeneo maalumu yaliyotengwa kuwapangia katika kufanya biashara zao
Mkuu wa wilaya huyo akifungua kikao amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Wamachinga wanafanya biashara zao katika hali ya utulivu na usalama ukilinganisha na maeneo ya kando za barabarani ambapo walio wengi ndipo hupanga bidhaa zao
Aidha mkuu huyo wa wilaya amewaonya matapeli wanaojipenyeza na kuwalaghai wamachinga kutaka wawapatie fedha kwa lengo la kuwapangia maeneo makubwa na upendeleo huku akisema zoezi hilo litaratibiwa chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo
Ameendelea kusema kwa sasa Manispaa ya Kigoma/Ujiji inakabiliwa na hali ya uchafuzi wa mji na kutupa taka ovyo katika mitalo ya barabara na maeneo yasiyo rasmi kutokana na uwepo wa baadhi ya Machinga na wateja wao kutupa taka kinyume na utaratibu
Amesema katika maeneo rasmi yaliyotengwa yanatarajia kujengwa miundombinu iliyoimara kama vile miundombinu ya vyoo, uwekwaji wa taa, na kujenga miundombinu ya kuweka taka katika maeneo hayo
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Frednand Filimbi akiwasilisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Machinga amesema maeneo hayo ni pamoja eneo la soko jipya linalojengwa jirani na standi ya Masanga, Soko la Mwasenga, eneo la Seremala Katubuka na eneo la Green belt jirani na Ofisi ya Kata ya Buzebazeba
Baadhi ya viongozi wa Machinga akiwemo Ali Jafari wa Soko la Mwanga na Manase Ruheta wa soko la Gungu wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kigoma kwa kikao hicho cha majadiliano huku wakiwamtaka katika kipindi cha kuwahamisha machinga hao utumike utaratibu mzuri pasipo kuwa na vurugu ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara hao kupimiwa maeneo pendekezwa pasipo kuingiliwa na wafanyabiashara wakubwa
Mkuu huyo wa wilaya mara baada ya kikao hicho amefanya ziara ya kutembelea machinga katika maeneo yao na kutembelea maeneo hayo yaliyotengwa akiwa na viongozi wa machinga maeneo husika
Kikao hicho cha Mkuu wa Wilaya na Viongozi wa Machinga kimehusisha Wenyeviti wa Masoko, Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya
Mkuu huyo wa wilaya amefanya kikao hicho mara baada ya Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwapanga Machinga katika maeneo stahiki yaliyo salama na yatayowakuza kiuchumi Nchi nzima
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa