Na Mwandishi Wetu
Katika kipindi cha miaka mitano inayoongozwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dr. John Pombe Magufuli ameweza kufanya miradi mingi katika kuboresha miundombinu ndani ya Manispaa yetu, hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu Mwailwa Pangani mapema wiki hii alipokuwa akifanya mahojiano na wandishi wa habari
Akiiongea kwa ujumla wake Mkurugenzi huyo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mabadiliko ya kiutendaji katika kuhakikisha maadili ya wafanyakazi yanaimarishwa, kusimamia miradi katika hali ya viwango na kupinga na kukataa Rushwa hali iliyofanya kukua na kuendelea kuboreshwa kwa miundombinu na kuweka mazingira mazuri katika shughuli za biashara, Kilimo na hata ufugaji katika Manispaa hiyo
Mkurugenzi huyo aliendelea kusema katika kipindi cha Miaka Mitano, Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kuboresha katika sekta ya Afya ambapo upatikanaji wa huduma za dharura zimeendelea kutolewa katika vituo vya afya ambapo katika kituo cha Afya cha Ujiji huduma ya Upasuaji imeendelea kutolewa huku kituo cha Afya cha Gungu ukarabati na ujenzi wa jengo la Upasuaji na Wodi ya wazazi ukiendelea kukamilika kwa fedha zilizotolewa na serikali hiyo kiasi cha Tsh Million mia mbili(200,000,000/=) huku wakazi wa Manispaa hiyo 448 wakiunganishwa na CHF iliyoboreshwa ambapo wanaweza kutibiwa katika vituo vyote vya Mkoa Mzima ukilinganisha na kwa Mwaka 2015 ambapo wanachama wa bima walitibiwa katika kituo cha afya au zahanati walizokatiwa bima hizo
Akitoa takwimu za uboreshaji katika sekta ya Elimu Mkurugenzi huyo alisema kwa kipindi cha serikali ya awamu ya tano Jumla ya madarasa sabini na tatu(73) , matundu ya vyoo mia moja ishirini na tano (125),Bwalo moja (1), na nyumba za walimu 4, ujenzi wa maabara 11 zikikamilika na maabara 46 zikiendelea kukamilishwa huku baadhi ya nyumba za walimu zilizopo shule ya Msingi Mgumile zikiunganishwa na mfumo wa umeme wa jua kwa upande wa Elimu Msingi ambapo jumla ya Billion 2,877,671,370.00/= zilitumika huku Jumla ya Tsh Million 250,959,030.00/= zikitumika upande wa Elimu Sekondari
Aidha aliiendelea kusema idadi ya wanafunzi wa awali walioandikishwa katika kipindi cha Awamu ya Tano imeongezeka kwa asilimia 124% kutoka wanafunzi 4000 kwa mwaka 2015 hadi kufikia wanafunzi 4949 mwaka 2020 na jumla ya wanafunzi 3288 walijiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 83 ukilinganisha mwaka 2015 ambapo wanafunzi 1732 sawa na asilimia 60 ndio waliojiunga na kidato cha kwanza
Akieleza miundombinu ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami alisema serikali imeweza kuboresha mitandao ya barabara za mitaani kwa kiwango cha lami ambapo jumla ya Km 13.75 zimejengwa kwa Gharama ya Tsh Billion 20.02/= ukilinganisha kwa kipindi cha awamu zingine zilizopita huku akiendelea kusema Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa barabara za mitaani katika kata zote kumi na tisa chini ya mamlaka ya TARURA ili kuweza kuboresha miundombinu na makazi ya wakazi wa Manispaa hiyo
Katika kuboresha sekta ya Mifugo na Uvuvi, Serikali ya awamu ya Tano imeweza kuboresha miundombinu katika Mwalo wa Kibirizi ambapo jumla ya Fedha za Kitanzania Jumla ya Tsh Million 447,292,077.00/= zimetumika katika ujenzi wa soko la kuuzia samaki, kuongeza chanja za kuanikia samaki na dagaa , mitamboo ya kuzalishia barafu kwa ajili ya kutunzia dagaa pamoja na ujenzi wa vyumba vya kuchakatia samaki kwa ajili ya usafirishaji ndani na nje ya Nchi ikiwa ni pamoja na ukarabati na uboreshaji wa Machinjio ambapo Jumla ya Tsh Million Hamsini (Tsh 50,000,000/=) zilitumika katika ukarabati huo
Alisema katika kuboresha maisha ya Wakulima Serikali imeanzisha sera ya uzalishaji wa Mbegu za Kisasa la Zao la Mchikikichi na kulitangaza kuwa zao la Kimkakati Nchini ambapo miche ya kisasa imeendelea kuzalishwa na kugawiwa kwa wakulima bure na jumla ya Miche Elfu thelathini (30,000) tayari imezalishwa na huku lengo likiwa ni kuzalisha miche Million moja kwa bajeti ya Tsh Million 300/=
Aidha Mkurugenzi huyo aliendelea kusema Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuboresha maisha ya makundi maalumu yanayopatikana katika jamiii na jumla ya vikundi 955 vilitambuliwa kufikia mwaka 2020 na kuwezeshwa mikopo isiyokuwa na riba na kukopeshwa Kiasi cha Fedha Tsh Million 267,777,500/= ukilinganisha kufikia mwaka 2015 ambapo vikundi vilikuwa vimekopeshwa kiasi cha Tsh Million 36,500,000/=
Aliendelea kusema mfuko wa maendeleo ya vijana umeongezeka kutoka Tsh Million 52,000,000/= kwa mwaka 2015 hadi kufikia Tsh Million 352,800,000/= kwa mwaka 2020 huku wanawake wakikopeshwa Tsh Million 164,900,000/= kwa vikundi 66 vya wanawake ukilinganisha na fedha iliyotolewa hadi kufikia mwaka 2015 ambapo ilikuwa kiasi cha Tsh million 22,400,000/= kwa vikundi 23 vya wanawake huku Wazee 4207 wameendelea kutambuliwa na kupewa matibabu bure katika vituo vya kutolea huduma za afya
katika kuboresha miundombinu ya viwanda na biashara masoko katika Manispaa hiyo yameendelea kujengwa huku mazingira ya kufanyia biashara kwa wajasiliamali na wanawake yakiboreshwa ambapo kiasi Cha Tsh Million 115,915,200.00/= zilitumika kujenga soko la samaki la jioni ambapo zaidi ya wafanyabiashara mia sita (600) wananufaika na uwepo wa soko hilo ukilinganisha kwa mwaka 2015 ambapo wafanyabiashara na wajasiliamali 350 walikuwa wanauzia bidhaa zao maeneo ambayo siyo rasmi
Jumla ya hekta 491 zimetengwa kwa ajili ya wawekezaji wa viwanda vikubwa na vidogo eneo la KIZES ambapo miundombinu ya umeme na barabara zinatarajiwa kuboreshwa kwa kiwango cha lami na hati 2,380 tayari zimeandaliwa na kutolewa kwa wananchi
Mkurugenzi huyo alihitimisha kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli na Serikali ya awamu ya Tano kwa kuonesha upendo wake kwa vitendo kwa Watanzania na Wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa kuendelea kuwapigania na kuboresha maisha yao kwa kipindi chote cha Awamu ya Tano huku mkurugenzi huyo akisifia suala la kukua na kuongezeka kwa makusanyo na mapato ya Manispaa hiyo.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa