Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu Mwailwa Pangani leo April 14, 2020 amefanya ziara katika manispaa hiyo katika kutatua malalamiko ya wananchi katika mitaa na makazi yao
Amefanya ziara baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wanaoingiliwa na maji na kuharibu miundombinu ya barabara za mitaani kutokana na wingi wa mvua inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma
Akiwa katika Mtaa wa Matofalini kata ya Kasingirima ambapo wananchi walikuwa na malalamiko ya kuharibika kwa barabara kutokana na wingi wa maji ya mvua amekutana na mwenyekiti wa mtaa huo Mhe. Abdallah Almas Mhuza na kumueleza namna wananchi wanavyopata shida kutokana na uharibifu wa barabara hiyo
Mkurugenzi huyo ameahidi barabara hiyo kujengwa kama nyongeza baada ya kuanza ujenzi wa barabara ya Kasulu-Ujiji kwa lengo la kuendeleza standi ya ndogo iliyopo katika eneo hilo na kusema barabara hiyo ipo tayari katika bajeti ya miradi itakayoanza baada ya mwezi July
Aidha mkurugenzi huyo ametembelea mtaa wa Airport ambapo ofisi ilipokea malalamiko ya ubovu wa barabara ya mtaa huo Airport -Mwasenga ambapo pia ametembelea barabara iliyoharibiwa na maji ya mtaa wa Masanga Kabingo ambapo maji yanawaathiri wananchi wa mtaa huo
Hata hivyo katika ziara hiyo Mkurugenzi huyo ametembelea daraja la Mto Katandara lililopo eneo la Bushabani kutokana na athari za mmomonyoko katika daraja hilo zilizojitokeza baada ya wananchi wa eneo hilo kuwa na tabia ya kuchimba mchanga
Mkurugenzi ameagiza wananchi kuacha tabia ya kuchimba mchanga katika eneo hilo kutokana na athari za mmonyoko ambazo zinaweza kuathiri makazi ya wananchi wa eneo hilo na kuathiri miundombinu ya barabara na daraja huku akimupigia simu Mhandisi wa TARURA kumtaka aje aone nakushughulikia haraka ili kuepuka kukatika kwa barabara hiyo
Katika ziara hiyo mkurugenzi amefika katika soko la samaki Kibirizi ambapo amekuta kilio cha wanawake wafanyabiashara wa Unga kuingiliwa na maji kutokana na kuongezeka kwa maji katika ziwa Tanganyika na kuathiri eneo wanalofanyia biashara ambapo mkurugenzi wa huyo amemtaka Mhandisi wa Manispaa hiyo Eng. Wilfred Shimba kusimamia ujazaji wa kifusi katika njia inayoleta maji na maji yaliyopo katika eneo hilo kuondolewa
Wanawake hao wafanyabiashara akiwemo Mama Tatu wamemshukuru Mkurugenzi huyo kwa ziara aliyoifanya na kujionea shida wanayokuwa wanaipata kutokana na maji hayo kujaa na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kulipa ushuru wa kila siku
Mkurugenzi huyo amehitimisha ziara yake kwa kutembelea ujenzi wa wodi ya Wazazi, na jengo la upasuaji unaoendelea katika kituo cha afya Gungu ambapo serikali imeingiza zaidi ya shilingi Milioni 200, katika uboreshaji wa kituo hicho, na kutembelea ujenzi unaoendelea wa ofisi ya kata ya Kitongoni ambapo kiongozi huyo amefanya ziara yake akiwa na Mchumi na Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa hiyo
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa