Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Mwailwa Pangani leo januari 3, amewasili katika shule ya msingi Kagera iliyopo katika halmashauri hiyo kwa lengo la kuona changamoto ya ukosefu wa vyoo inayoikabili shule hiyo
Akiwasili katika shule hiyo akiwa na wataalamu wake Mkurugenzi huyo alipewa taarifa na mwalimu mkuu wa shule hiyo Ndugu. Faustino Satula na kusema shule hiyo ina jumla ya matundu mawili (2) ya vyoo huku jumla ya wanafunzi waliopo shuleni hapo wakiwa ni wasichana 634 na wavulana 569 na kufanya jumla ya wanafunzi 1203 sawa na uwiano wa tundu moja kwa wanafunzi 601
Ameendelea kusema upungufu wa vyoo hivyo unafanya uchafuzi wa mazingira kwa baadhi ya wanafunzi kujisaidia ovyo katika maeneo yasiyo sahihi huku wanafunzi wengine wakienda kujisaidia katika nyumba jirani za wananchi wanaoizunguka shule hiyo na kuleta kero kwa wakazi hao
Mwalimu mkuu hiyo ameendelea kutoa taarifa kuwa hali ya miundombinu ya shule hiyo ni mibovu na ya zamani, hali ambayo haiwavutii wanafunzi ili waweze kuendelea kujifunza katika mazingira hayo huku akimuomba Mkurugenzi huyo aipe kipaumbele katika ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo
Naye mkurugenzi wa halmashauri hiyo akiwa katika shule hiyo amesikitishwa na miundombinu ya shule hiyo na ukosefu wa vyoo huku akimuagiza Mhandisi wa halmashauri siku ya kesho kumpeleka fundi ujenzi ili kutathimini gharama za ujenzi wa choo kipya chenye matundu kumi ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira salama
Mkurugenzi huyo amesema “Mhandisi nakuagiza kesho mlete fundi ,watathimini ujenzi wa choo kipya chenye matundu kumi ya kuanzia , maana mahitaji yote ya hapa kama ni mchanga,tofali na fedha iko ndani ya uwezo wetu na kufikia siku ya jumatano ujenzi uanze mara moja “
Mkurugenzi huyo ameendelea kumtaka mhandisi huyo kufanya tathimini ya ukarabati wa majengo , kutokana na uchakafu wa sakafu madarasani, na uchakavu wa mabati ya shule hiyo ili kuweza kuboresha mazingira ya walimu na wanafunzi katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji
Mkurugenzi huyo ameahidi kupeleka tofali, simenti na fedha ili kuanza na ujenzi wa choo hicho haraka, na kusema katika ukarabati wa madarasa hayo itafanyika tathimini kutoka katika taarifa ya mhandisi kwa lengo la kuangalia mahitaji ya kuingiza katika bajeti ili majengo ya shule hiyo yaweze kuboreshwa
Akiwa katika ziara hiyo shuleni hapo ameongea na walimu na wanafunzi wa shule hiyo, maeneo mengine aliyofanya ziara ni katika bwawa la Katosho ambapo imeanzishwa kitalu cha miche ya kisasa ambapo jumla ya miche elfu nane ipo tayari huku lengo likiwa ni miche elfu thelathini
Aidha ameendelea na ziara yake katika machinjio ya kibirizi ambapo machinjio hayo kwa mwaka 2013 yalifungwa na mamlaka ya vyakula na dawa (TFDA) kutokana na kutokidhi vigezo , ambapo mkuu wa Idara ya Uvuvi na Mifugo Ndugu. Edmund Kajuni ameeleza machinjio hayo yamekamilika katika ukarabati huku akisema kwa sasa yako tayari katika kuanza kutumika kuchinjia wanyama
Ameendelea kusema machinjio hiyo ipo tayari kuanza kutumika kutokana na vigezo iliyofungiwa vyote kurekebishwa na kusema kwa wiki ijayo matarajio ya kuanza kwa machinjio hayo ni makubwa sana na wanatarajia kuanza kuchinja Ng’ombe kumi na tano (15) hadi kumi na tisa (19) kwa siku.
Mkurugenzi huyo amehitimisha ziara yake katika shule ya sekondari Rubengera(tarajiwa) awali iliyokuwa shule ya Msingi Kigoma ili kukagua ukarabati wa majengo unaoendelea na kuwakuta mafundi wakiendelea na kazi huku akiwataka kufanya kazi usiku na mchana ili mapema mwezi march wanafunzi wakidato cha kwanza waweze kuanza masomo yao.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa