Na Mwandishi wetu
Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji jana May 5, 2021 ilifanya mkutano na wafanyabiashara wa soko la Mwanga lililopo katika Manispaa hiyo kwa lengo la kujadili changamoto zilizopo katika soko hilo
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Frednand Filimbi akifungua Mkutano huo alisema lengo la kikao hicho ni pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili na kuwa na mazingira bora kwa wafanyabiashara
Akizungumzia changamoto ya kuwepo kwa taka mda mrefu alisema tayari ofisi imeweka utaratibu wa Ukusanyaji taka kwa idara ya afya na mazingira kwa kuwawezesha lita mia nne (400) za mafuta kila wiki na kuhakikisha taka zote zinapelekwa katika dampo la kisasa la Msimba
Aliendelea kusema changamoto ya kukosekana kwa maji mara kwa mara inatafutiwa ufumbuzi kwa kuongea na mamlaka zinazohusika na Maji Kuwasa ili maji yawepo mda wote kutokana na kuhudumia wafanyabiashara wengi ili kuepuka mlipuko wa magonjwa unaoweza kutokea
Kaimu Mkurugenzi huyo aliwataka wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu kwa kulipa kodi na tozo zinazotozwa kwa mjibu wa sheria na kufanya hivyo kutaepusha usumbufu kwa wafanyabiashara hao
Naye mwenyekiti wa soko la Mwanga Ndugu. Raymond Ndabhiyegetse akiongea aliipongeza ofisi ya Mkurugenzi kwa kuanzisha utaratibu wa kuongea na wafanyabiashara kwa kusikia kero na changamoto zao na kusema kuendelea kufanya hivyo kutaukuza uchumi wa wafanyabiashara na kukua kwa mji huo
Mwenyekiti huyo aliendelea kuwataka wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi, tozo na ushuru wanaotakiwa kulipa kwa mfanyabiashara ili kuepuka migogoro baina yao na Halmashauri na kufanya mfanyabiashara mmoja mmoja kukua kiuchumi na kufikia malengo yake
Naye mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo Ndugu. Jafari Saidi aliipongeza ofisi ya Mkurugenzi kwa mkutano huo wa kujadili changamoto za wafanyabiashara na kuendelea kusema wao kama wafanyabiashara watapendezwa kama vikao hivyo vitakuwa mara kwa mara ili kuimarisha na kukuza uchumi wao
Soko la Mwanga ni moja wapo ya masoko saba (07) yaliyopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji ikiongoza kwa mapato ya Halmashauri ikifuatia soko la Kigoma Mjini, Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji tayari imejenga majengo mawili ya wajasiriamali (machinga) na wafanyabiashara wa Mahindi yakigharimu fedha za Kitanzania Million themanini na laki saba na elfu sita (Tsh 80,706,000/=)
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa