Wenyeviti wa Mitaa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji wameahidi kutatua changamoto ya wanafunzi kukosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka mwaka 2020 kutokana na upungufu uliopo katika halmashauri hiyo wa vyumba vya madarasa 38 kwa kuwashirikisha wananchi
Wameyasema leo Desemba 19, katika ukumbi wa halmashauri baada ya wenyeviti wa mitaa 68, watendaji wa kata na mkurugenzi wa halmashauri kukutana kwa lengo la kunusuru wanafunzi 1753 waliofaulu na kukosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na upungufu wa madarasa katika shule za upili.
Akitoa ufafanuzi katika kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndugu. Frednand Filimbi amesema wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2019 ni wanafunzi Elfu tatu mia tisa kumi na nane (3918) sawa na 85% ya waliofanya mtihani, waliochaguliwa kujiunga na na kidato cha kwanza kwa shule zilizopo ni wanafunzi Elfu mbili mia moja sitini na tano (2165) ambapo wanafunzi waliofaulu na kukosa nafasi kutokana na Upungufu wa vyumba vya madarasa ni wanafunzi Elfu moja mia saba hamsini na tatu (1753) na kufanya kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa thelathini na nane(38) kwa sasa ili wote waweze kujiunga na kidato cha kwanza
Ameendelea kusema tayari halmashauri imechukua hatua kukabiliana na tatizo hilo kwa kuanza mchakato wa ununuzi wa tofali na kukutana na baadhi ya Taasisi za serikali na binafsi kama vile Benki ya NMB ili kuweza kusaidia katika kuhakikisha halmashauri inaondokana na upungufu huo wa vyumba vya madarasa
Naye Kaimu Afisa Elimu Sekondari Ndugu. Yaragwila Gwimo amesema halmashauri ina shule 18 za kutwa, na shule 1 ya Bweni ambapo shule 8 hazina upungufu wa madarasa na shule 10 kuwa na upungufu wa madarasa
Ameendelea kusema kata ya Gungu inaongoza kwa kuwa na wanafunzi mia nne hamsini na mbili (452) waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza sawa na vyumba vya madarasa tisa (9) vinavyohitajika ikifatiwa na kata ya Mwanga kaskazini yenye wanafunzi mia tatu sabini na mbili (372) waliokosa nafasi sawa na vyumba vya madarasa saba(7)
Naye Afisa Tarafa wa Kigoma Kaskazini Ndugu. Maxmilliani Ngasa amepongeza kikao hicho kilichoandaliwa na ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri huku akiwataka watendaji wa kata, wenyeviti wa mitaa hiyo kwenda kulifanyia kazi kwa kuliweka kuwa agenda za kata na kufanya mikutano na wananchi kwa lengo la kutatua tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa
Nao baadhi ya watendaji wa kata akiwemo Wamesema ujenzi wa vyumba vya madarasa wameupokea kwa uzuri na kuahidi kulifanyia kazi kwa kufanya mikutano na wananchi , na kusimamia shughuli ya ujenzi itakayokuwa ianendelea ili kuhakikisha wanafunzi waliokosa nafasi wanaanza masomo yao kabla ya mwezi februali
Nao baadhi ya wenyeviti wa mitaa akiwemo Ndugu Azizi Ibrahimu (myenyekiti wa mtaa wa Mgeo,Buhanda) na Bakari Songolo (Mwenyekiti wa mtaa wa Taifa, Rusimbi) wameipongeza halmashauri ya Manispaa kwa kuja na mpango mkakati wa ujenzi wa madarasa kwa kushirikiana na nguvu ya wananchi kuweza kufanya wanafunzi walifaulu wanapata nafasi ili kuweza kuendelea na masomo ya upili
Naye mwenyekiti wa mtaa wa Kasulu Ndugu. Mlekwa Mfaume ameendelea kupongeza halmashauri kuja na mpango wa wanafunzi waliokosa nafasi ili wapate fursa ya kujiunga na masomo hayo ya upili huku akishauri halmashauri iandae mkakati wa kujenga nyumba vya madarasa mapema kabla ya wanafunzi kukosa nafasi na kuchelewa kuanza masomo yao
Naye Kaimu Mkurugenzi amehitimisha kwa kuwashukuru Wenyeviti wa mtaa, na watendaji wa kata kuitikia wito na kuonesha nia ya kuweza kujenga vyumba vya madarasa kwa kushirikiana na nguvu ya wananchi ili kuweza kurithisha elimu katika kizazi kilichopo, na kusema serikali ya awamu ya tano ipo pamoja na wananchi kuhakikisha elimu inakuwa urithi kwa watoto wa Kitanzania na kusema Manispaa ya kigoma/Ujiji ilishika nafasi ya 1 kimkoa na ya 72 kitaifa kwa ufaulu wa asilimia 85% katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba 2019
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa