Na Mwandishi Wetu
Baraza la Madiwani Manispaa ya Kigoma/Ujiji limeridhia wafanyabiashara wa soko la Mwanga kupisha ujenzi wa soko hilo kisasa hadi kufikia June 30, 2022 na kuhamia soko la jipya la Masanga lililotengewa
Baraza hilo lililofanyikia ukumbi wa Manispaa hiyo leo May 18, 2022 limeridhia mara baada ya Meya na Mwenyekiti wa baraza hilo Mhe. Baraka Naibuha Lupoli kuruhusu Wàheshimiwa Madiwani kupiga kura ili ujenzi kufanyika katika soko hilo
Meya na Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema kujengwa kwa soko hilo kutaboresha mazingira ya wafanyabiashara Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa kukuza mapato ya ndani na kuvutia wawekezaji kibiashara
Ameendelea kusema kujengwa kwa soko hilo kisasa kutaboresha Mandhari (mwonekano) na kupendezesha na kukuza usafi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji
Akihutubia baraza hilo Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bi. Ester Alexander Mahawe amelipongeza Baraza la Madiwani kwa uamuzi waliofanya kutokana na mpango wa kuanza ujenzi wa soko ili kuboresha Mazingira yatakayokuza uchumi wa Wafanyabiashara na wakazi wa Manispaa hiyo
Ameendelea kuwataka wafanyabiashara wa soko hilo kuitikia wito wa kuondoka mapema kabla ya tarehe iliyopangwa na kuhamia soko jipya la Masanga ambalo wametengewa kufanya biashara zao katika kipindi chote cha ujenzi wa soko hilo la Mwanga kisasa
Mkuu huyo wa Wilaya amehitimisha kwa kulitaka Baraza la Madiwani kuanza kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuanza ujenzi wa soko la Kigoma Mjini ili kuendelea kuboresha maisha ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kutokana na manufaa ya ujenzi huo
Naye Diwani wa Kata ya Kasingirima Mhe. Abdallah Kiembe amesema kuanza kwa ujenzi huo kutakuza uchumi na kuboresha huduma bora kwa Wananchi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa kuinua vipato vyao
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kigoma Ndugu. Alhaji Yassini Mtalikwa amesema chama hicho kinaridhishwa na utendaji kazi wa baraza hilo la Madiwani huku akisema hawatavumilia viongozi wowote wanaohujumu na kukwamisha miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji
Awali Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Athumani Msabila akiwasilisha taarifa amesema Soko la Mwanga linatarajiwa kujengwa kisasa Mapema kuanzia mwezi July, Mwaka huu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) kupitia mradi wa TACTICS huku akisema tayari wafanyabiashara wameshaarifiwa kuhamia soko la Masanga ili kupisha ujenzi huo kabla ya June 30, 2022 na Miundombinu ya Maji, Umeme, na Umeme inaendelea kukamilishwa
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa