Moja ya mkazi wa Bangwe aliyebainishwa kwa kutokuwa na vyoo kabisa akianza taratibu za ujenzi baada ya kukutana na maafisa afya nyumbani kwake
Kaimu mkuu wa idara ya usafi, afya na mazingira manispaa ya Kigoma Ujiji akikagua moja ya choo kilichopo katika mtaa wa kamala Kata ya Bangwe
Zoezi la ukaguzi kwa watu wasio na vyoo manispaa ya Kigoma Ujiji laanza katika kata ya Bangwe leo January 24, kwa kutoza faini kutokana na agizo la Waziri mkuu Kassimu Majaliwa kila nyumba kuwa na choo bora.
Agizo hilo lililotolewa na kiongozi huyo mwishoni mwa mwaka 2018 ikiwa ni kuleta uimarishaji wa afya za Watanzania, kutokana na agizo hilo manispaa ya Kigoma Ujiji kupitia kitengo chake cha Usafi na Mazingira chini ya kaimu mkuu wa kitengo hicho Ndugu. Bakari A. Bakari imefanya oparesheni kwa kutembea nyumba kwa nyumba na kubaini na watu wasio na vyoo.
Akizungumuza kaimu mkuu wa kitengo hicho Manispaa ya Kigoma/Ujiji amesema oparesheni hii itafanyika katika nyumba zote zilizo katika kata 19 zilizobainishwa kutokuwa na vyoo na mawakala wa kuleta mabadiliko ya jamii (CCA).
Ameendelea kusema katika ukaguzi huo unafanyika ni pamoja na kutoa elimu namna vyoo bora vinatakiwa viwe kwa kuhakikisha vyoo vinakuwa na shimo la pembeni lililojengewa, lenye paa, na kuwa mlango na kuwa na vibuyu chirizi na sabuni ili kuimarisha usafi wa mikono na mwili mara baada ya kujisaidia.
Katika ziara hiyo Shilingi elfu hamsini zimekusanywa kutokana na faini ya mtu mmoja ambaye hakuwa na choo na wengine zaidi ya kumi na tano kupewa masaa ishirini na nne kulipa faini hiyo katika ofsi ya kata na kuhakikisha vyoo vinajengwa ndani ya siku saba.
Naye kiongozi wa mawakala wa kuleta mabadiliko katika jamii(CCA) Bi. Yasinta Vitusi amesema tayari wamebaini nyumba 98 zilizopo katika manispaa ya Kigoma Ujiji ambazo hazina vyoo kabisa na zingine kutokuwa na vyoo bora.
Ameendelea kusema katika ukaguzi huo wameendelea kutoa elimu juu na umuhimu wa vyoo kwa kuwataka wakazi wa manispaa ya Kigoma Ujiji kuimarisha afya zao kupitia kampeni ya “nyumba ni choo” ili kuepuka magonjwa ya kipindupindi na tumbo.
Nao baadhi ya wananchi waliobainishwa kwa kutokuwa na vyoo waliweza kuelezea zoezi hilo, Bi. Raila Habibu mkazi wa kata ya Bangwe anasema zoezi hilo ni zuri kwani linawaepusha na kuwapa elimu namna ya kuepukana na magonjwa na kuahidi choo chake kukishughulikia ndani ya siku saba alizopewa.
Naye mzee Amiri Barakiliza aliyebainika kwa kutokuwa na choo amesema changamoto ya wakazi wa kata hiyo kutokuwa na vyoo ni uzembe hali inayoweka afya zao katika mazingira hatarishi kwa kukumbwa na magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu na kuahidi na kuchimba choo ndani ya siku saba katika kaya yake.
Akihitimisha zoezi hilo kaimu mkuu wa kitengo cha Usafi na Mazingira Ndugu. Bakari A. Bakari amesema zoezi hilo ni endelevu na wataendelea kulifanya kwa kata zote ambazo wakazi ambao tayari wameshabainishwa kutokuwa na vyoo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka ofsi ya Mkurugenzi wa halmashauri, watendaji kutoka katika kata na mawakala wa kuleta mabadiliko ndani ya jamii.
PICHA ZAIDI INGIA KATIKA MAKTABA YA PICHA
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa