Na Mwandishi wetu
Watendaji wa kata za Manispaa ya Kigoma/Ujiji wametakiwa kuzijengea uwezo Asasi za kijamii (vikosi kazi) zinazojihusisha na shughuli za usafi wa Mji katika mitaa mbalimbali ili ziweze kujitegemea na kujiendesha kifedha
Yamesemwa hayo leo April 1, 2021 na Mtaalamu wa udhibiti taka ngumu na Mazingira Ndugu. Patrick Matandala wakati akihitimisha mafunzo yaliyofanyika kwa siku mbili kwa Watendaji Kata katika ukumbi wa Hoteli ya Greenview katika kuwajengea uwezo wa kuhakikisha mji unakuwa safi
Mtaalamu huyo amewataka watendaji kata kuhakikisha wanazishauri asasi za kijamii (vikosi kazi) zinazojishughulisha na usafi kwa kuhakikisha zinajiendesha ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa na ukusanyaji wa pesa za uzoaji taka ili ziweze kukua na kufikia hatua ya Makampuni ya usafi
Ameendelea kusema kuwa ipo haja ya asasi hizo kusajiliwa na kupewa mikataba ya usafi ili iweze kuwalinda katika shughuli wanayoifanya na kusajiliwa huko kutasaidia asasi hizo kuwa na uwezo wa kukopeshwa katika taasisi mbalimbali za kifedha au makampuni kwa kuwezeshwa vifaa vya usafi
Amesema asasi hizo za kijamii kama zitawezeshwa na kujengewa uwezo zitakuwa na uwezo wa kuchakata baadhi ya taka ili zitumike kama bidhaa zingine na utengenezaji wa mbolea za mboji(recycling and re-use) ambapo amesema vikundi vingine vimeanza kukusanya taka za plastiki na kuzisaga na kuzisafirisha kwenda viwandani
Kaimu Mkuu wa idara ya Usafi na Mazingira Ndugu. Elishaphati Rusemvya amewapongeza watendaji hao kwa mafunzo ya kujengewa uwezo waliyoyapata ili kuhakikisha wanakuza asasi za kijamii na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kuhakikisha mji unakuwa safi na taka nyingi kukusanywa ili kuepuka madhara yatokanayo na kusambaa kwa taka katika jamii
Mkuu huyo wa idara amewakaribisha wadau mbalimbali wa kufanya usafi wa mji kutokana na fursa za kujiingizia kipato, na upungufu wa asasi za usafi na kwa sasa vikundi vilivyosajiliwa ni vikundi ishirini na mbili(22) tu vitakavyofanya usafi kwa mitaa hiyo ishirini na mbili(22) licha ya Manispaa hiyo kuwa na mitaa sitini na nne(64)
Amesema kwa mjibu sheria ndogo za Manispaa hiyo suala la uchimbaji wa shimo majumbani ili kuwekewa taka ni kosa kisheria hivyo wakazi,taasisi na wafanya biashara wanawajibu wa kukusanya taka wanazozizalisha na asasi za kijamii zinazojishughulisha na usafi kuzichukua na kuzipeleka katika maeneo yaliyopangwa kwa ukusanyaji wa taka kwa kila mtaa
Mtendaji wa kata ya Rubuga Bi. Asha Mrisho amesema mafunzo hayo waliyoyapata yamewajengea uwezo wa kuhakikisha wanazisaidia asasi za kijamii zinazojishughulisha na usafi wa mji kwa kila mtaa, na wao watahakikisha wanashiriki kuzikuza huku agenda za usafi wa mazingira kuwa suala mtambuka kwa mwananchi wote na kuhakikisha wanashiriki katika kutoa ada za ukusanyaji wa taka hizo
Mafunzo hayo yaliyofanyika ikiambatana na ziara ni mwendelezo wa kujengea uwezo wa wataalamu ambapo awali yalifanyika kwa Wakuu wa idara na Vitengo na yanatarajiwa kuendelea kwa wadau mbalimbali ikiwemo asasi za kijamii(vikosi kazi vya usafi) zinazoshighulisha na usafi wa mji ili kuhakikisha zinakuwa na uwezo wa kujiendesha
Na ikumbukwe Manispaa ya Kigoma/Ujiji inazalisha tani mia moja na arobaini (140) kwa siku ambapo inakadiriwa kila mkazi wa Manispaa hiyo kwa siku anazalisha kilogram 0.5 kwa siku na hali hiyo inatokana na ukuaji na ongezeko la watu
Picha na video zaidi ingia katika maktaba ya picha katika tovuti yetu www.kigomaujijimc.go.t
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa