Kongamano la kuhitimisha wiki ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Manispaa ya Kigoma/Ujiji limefanyika leo march 5, katika ukumbi wa Redcross uliopo katika Manispaa hiyo
Kongamano hilo limefanyika likianza kwa maandamano ya wanawake wakianzia Ofisi kuu ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kupitia barabara ya Lumumba , Maweni , kituo cha Polisi hadi ukumbi wa Redcross wakiwa na ujumbe wa kuhamasisha usawa na haki sawa kwa wote
Katika kongamano hilo Wanawake wameaswa kuwa katika haki wanazopata isiwe nafasi ya kuweza kuwagandamiza wanaume katika familia zao bali ikawe mwanzo wa kufungua fursa za kiuchumi ili kuleta ustawi wa kifamilia katika Nyanja tofauti tofauti
Akihutubia katika kongamano hilo Mgeni Rasmi Bi. Frida Chinuka amepongeza jitihada zilizofanyika Nchini na zinazoendelea kufanyika kuinua uchumi kwa wanawake kupitia asasi na Mashirika mbalimbali ya Serikali na yasiyo ya Serikali
Katika hotuba yake amewataka Wanawake kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali pasipo kujinyanyapaa huku wakiamini kuwa wanawake wanaweza na jamii inapaswa kuwapa nafasi ili waweze kuachana na utegemezi wa kifikra na uchumi pia
Ameipongeza Halmashauri ya Manispaa kwa kuhamasisha na kuunda vikundi 65 vya Wanawake wajasiliamali na kuwawezesha kupata mikopo kutoka katika mikopo ya wanawake , vijana na walemavu inayotolewa na Manispaa ya Kigoma/Ujiji mara kwa mara huku akisisitiza Manispaa hiyo kuendelea kuwainua na kuwaendeleza wanawake kiuchumi
Naye Mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Vijana , Wazee na Watoto Ndugu. Jabiri Majid akieleza mafanikio ambayo Manispaa hiyo imeweza kufikia katika kuwainua wanawake amesema Manispaa imekuwa ikitoa elimu ya kijinsia , na kupambana na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanawake na watoto
Ameendelea kusema Manispaa imeunda kamati za ulinzi za kupambana na ukatili na kuleta usawa wakinjisia , kamati hizi zimeundwa kwa kata kumi na tisa (19) zote za manispaa ya Kigoma/Ujiji na kutengeneza mazingira ya kibiashara kwa wanawake kwa kuanzisha soko la usiku la Mwanga
Jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia na watoto Mkoani Kigoma limesema limekuwa likipambana na vitendo vya kiutali vinavyofanywa na jamii huku wakiipongeza jamii kwa kutoa ushirikiano mara kwa mara licha ya baadhi ya watu wachache kuwaficha waharifu na wengine kutotoa ushahidi wa waharifu
Afisa kutoka Jeshi la Polisi akitoa tawimu amesema kwa mwaka 2018 watu waliolipotiwa kubaka walikuwa watuhumiwa 22 huku kwa mwaka 2019 wakiongezeka na kufikia watuhumiwa 23, na vitendo vya ulawiti vilivyolipotiwa ni matukio mawili (2) tangu mwezi januari 2020 huku matukio ya kujaribu kubaka yakiwa mawili(2)
Amehitimisha kwa kuitaka jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kulipoti vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto , na wale wanaoficha waharifu kwa kigezo cha kuwa ni ndugu au kuogopa kutoa ushirikiano kuacha tabia hiyo ili kuweza kumaliza vitendo vya ukatili vinavyofanyika ndani ya jamii
Naye mwakilishi kutoka Shirika la kuhudumia viwanda vidogo(SIDO) Bi. Mwaselembe amewapongeza wanawake wote wajasiliamali wadogo na wakubwa kwa kuendelea kujiinua kiuchumi huku akiwataka wanawake wote kuungana pamoja katika shughuli zao na kuanzisha viwanda vidogovidogo
Amewataka wanawake kujenga tabia za kushindana katika bidhaa zao na kuwa wabunifu ili kuleta mvuto tofauti tofauti kwa wateja wao na wanawake hao kuzalisha kulingana na mahitaji ya jamii ili kuweza kufurahia biashara ambazo wanazifanya
Naye Afisa Masoko kutoka Benki ya NBC Bi. Janeth Chacha ameendelea kutoa pongezi kwa wanawake kuendelea kuona fursa za mikopo zinazokuwa zikitolewa katika benki mbalimbali , huku akiwataka wanawake kujenga tabia ya kuweka akiba katika uzalishaji wao wanaoufanya
Akiongea katika kongamano hilo Bi. Chausiku Mgahula amesema zipo mila za wanawake wa kigoma zinazowaathiri ambazo mila hizo ni wanaume kuwa na tabia ya kusafiri kwenda mikoa mingine kutafuta pesa maarufu “Kuhanzura “ na kuwaachia watoto bila matunzo yeyote jambo linalowathiri wanawake katika malezi ya familia kutokana na vipato vidogo wanavyovipata huku akiwaasa wanaume wanaposafiri kwenda mikoani kuzikumbuka familia zao katika mahitaji ya kila siku
Kongamano hilo la wanawake limefanyika ikiwa ni katika kuelekea kilele cha siku ya wanawake Duniani ambapo huazimishwa March 1-8 kila mwaka, ambapo maadhimisho ya mwaka huu yakiwa na kauli mbiu ya “Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa nay a baadae” na kwa mwaka huu Kitaifa maadhimisho hayo yakihitimishwa mkoani Simiyu
Maadhimisho haya ya Siku ya wanawake Duniani yalianzishwa mwaka 1911 huko nchini Marekani ambapo wanawake wafanyakazi wa viwandani walikuwa wakinyanyaswa na kuamua kuanzisha siku hii ili kudai haki sawa kwa wote na Nchini Tanzania maadhimisho hayo yalianza mwaka 1997
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa