Na Mwandishi wetu
Wadau wa Usafi na mazingira leo Desemba 29, wamekutana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji katika Ukumbi wa Manispaa hiyo kwa lengo kuweka mikakati ya kufanikisha Mji unakuwa safi
Wadau hao waliofika katika Ukumbi wa Manispaa ni Watendaji wa Kata, wenyeviti wa serikali za Mitaa, kamati za Usafi ngazi ya Mtaa, Viongozi wa Dini, na vikosi kazi vya usafi vilivyosajiliwa ngazi ya mtaa wakiongozwa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo
Mkuu wa idara ya Mipango na Uchumi Ndugu. Frednand Filimbi Akiwasilisha kwa niaba ya Mkurugenzi amesema lengo la kuwaita wadau hao ni kuweka mikakati imara ya kuendeleza Usafi wa Mazingira kwa Mitaa 68 ya Manispaa na kuhakikisha mji unakuwa safi kwa kutumia vikosi kazi
Mkuu huyo wa idara ameendelea kusema ni wajibu wa vikosi kazi vilivyoundwa ngazi ya mtaa kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao ambapo watakuwa wakikusanya taka katika maeneo maalumu yaliyotengwa huku Magari ya Manispaa yakiondoa taka hizo kwa kuzipeleka dampo la kisasa eneo la Msimba
Aidha Mkuu huyo wa idara amesema kwa mjibu wa sheria ni wajibu watu wote kuchangia tozo za kuondoa taka Mjini na katika Makazi ya watu kutokana na kila mmoja kuwa chanzo cha uzalishaji taka, na tozo hizo hutolewa kwa kila kaya, taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kwa kila mwezi
Suala la kuzagaa kwa mifugo ya Mbuzi katika ya mji ni moja ya jambo ambalo limejadiliwa kwa kina ambapo imeonekana kuwa Mifugo hiyo imekuwa mingi katika Manispaa hiyo na kuzagaa ovyo ambapo Mkuu huyo wa idara amepiga marufuku na kuwaonya wafugaji huku akisema kwa mjibu wa sheria ni marufuku kufuga Mifugo mjini inayozagaa ovyo mtaani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wafugaji na Mifugo hiyo kupigwa mnada
Mkuu huyo amehitimisha kwa kuwataka watendaji wa Kata na Mitaa kusimamia vikosi kazi hivyo vya Usafi kwa kila mtaa huku wenyeviti wa mitaa na kamati za Usafi katika mitaa zikitakiwa kuwa hamasa kwa jamii ili kuendeleza Usafi wa mji na kuepuka na milipuko ya Magonjwa yatokanayo na uchafu
Naye Mjumbe wa kamati ya Usafi mtaa wa Uwanja wa Ndege Bi. Donatila Mzaira amepongeza kuandaliwa kwa kikao hicho kwa lengo la kujadili Usafi wa mji huku akisema yupo tayari kuihamasisha jamii kwa ajili ya kuhakikisha mji unakuwa safi na kutekeleza sheria za Usafi katika jamii inayomzunguka
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisangani Abdallah Kimenya amesema tayari kikosi kazi katika mtaa wake kipo tayari kikiendelea kwa Usafi ambapo kila kaya hutoa fedha za Kitanzania kila mwezi Tsh 1000/= na hadi sasa mtaa huo umekuwa safi licha ya Changamoto za uwali za taka kuwa nyingi mtaani huku akiomba Ofisi ya Mkurugenzi kuongeza kizimba cha kukusanyia taka
Naye kiongozi wa dini na Mchungaji Linus Simoni ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji kwa jitihada za kuendeleza Usafi wa mji huku akisema wao kama viongozi wa dini wapo tayari kuhamasisha waumini na washirika wa imani zao ili kushiriki katika Usafi wa mji na kuhamasisha vijana na makundi mbalimbali kuchukua fursa ya kujiajiri kupitia Ukusanyaji taka katika Manispaa hiyo
Aidha wadau hao wamekubaliana kwenda kuanza shughuli ya kukusanya taka kwa kuishirikisha jamii, taasisi za Serikali na zisizo za Serikali ambapo vikosi kazi hivyo vya Usafi kuchukua asimilia sitini(60%) ya Makusanyo huku Ofisi ya Mkurugenzi ikibaki na asilimia arobaini (40%) ya Makusanyo hayo na wadau hao wamepanga kukutana kwa kikao kingine cha tathimini mapema Mwezi Marchi 2021
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa