Wakazi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji wameahidi kutowavumilia wale wote watakaokuwa waharifu wa miundombinu ya barabara iliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia chini ya mradi ya uendelezaji wa kimkakati wa miji na majiji Tanzania (TSCP)
Wameyasema hayo katika mikutano tofautitofauti iliyofanyika na inayoendelea katika kata zilizopitiwa na miradi hiyo ya barabara inayoendeshwa na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo juu ya uthamani, umiliki na utunzaji wa miundombinu hiyo
Akiongea katika mkutano uliofanyika jana Januari 20, mmoja wa wananchi wa kata ya Kagera Ndugu. Emmanueli Kinyota alipongeza wafadhili wa miradi hiyo, Serikali ya awamu ya tano kwa kuidhinisha miradi hiyo kujengwa manispaa ya Kigoma/Ujiji huku akiwapongeza pia wataalamu kwa kutoa elimu namna gani wanawanchi wataweza kutumia na kutunza miradi hiyo
“wakazi wa Kagera ni neema kwetu kwa mradi huu wa barabara na umeleta mabadiliko makubwa kwa mji wetu huu, kila siku tunapokea wageni kuja kutafuta ardhi,ni kwa mara ya kwanza daladala zinafika eneo letu hili, bajaji nazo zinafika huku, watu wanakuja kutafuta matunda kwa soko letu hilo, hivyo nasema tutapambana na watu wa kuiba taa, madereva wote wanaomwaga oili barabarani na dereva wa bodaboda wanaoburuza vyuma vyao na kupiga baruti, nasema tutawatafuta hadi uvunguni na tutawapata”
Naye Bi.Amina Mahelela alisema “ Na sisi wanawake tutakuja kwa mtendaji kumtaarifu wale wote ambao ni waharibifu wa barabara zetu, na tutakuwa tunawataja majina lakini na nyie mje mturudishie maji mliyoyakata kipindi mnajenga”
Naye Afisa Usafi na Mazingira wa Manispaa hiyo Ndg. Elishaphati Rusemvya akitoa elimu hiyo kwa wakazi wa kata ya Kagera katika Ofsi ya Mtendaji wa Kata hiyo alisema wananchi wote wana wajibu wa kuilinda miundombinu ya barabara hiyo iliyojengwa na kutambua barabara hizo ni miliki yao na endapo uhalibifu wowote utatokea atakayeathirika ni wananchi wanaotumia barabara hizo
Alisisitiza juu ya madereva kutumia barabara hizo kwa utaratibu ,kuendesha kwa kutoenda kwa kasi kubwa na kutomwaga oili endapo atabainika mtu kwa mjibu wa sheria atalipa faini ya shilingi milioni moja(Tsh 1,000,000/=) lakini pia kuepuka utiririshaji wa maji machafu katika mitalo iliyojengwa na atakayebainika atalipa faini ya shilingi elfu hamsini (Tsh 50,000/=) na isiyozidi shilingi laki mbili (Tsh 200,000/=) huku akisisitiza utunzaji wa miundombinu hiyo.
Naye Afisa Ustawi wa jamii Bi. Agnes Punjila akiwasilisha mada katika mkutano huo alisema ujio wa barabara hizo ni maendeleo kwa wakazi wa eneo husika na katika matumizi ya miundombinu hiyo lazima tuzingatie usalama wa wanawake, watoto na wazee
Alisema “barabara hizi isiwe majanga na misiba kwa watoto wetu, jamii nzima ina wajibu wa kuwalinda watoto na kuwapa tahadhari namna ya kupita katika barabara hizi na kizuri zipo pia njia za watembea kwa miguu zimetengenezwa kando ya barabara kubwa hivyo lazima tuzingatie matumizi hayo pasipo mwingiliano lakini pia tukiangalia usalama wa wazee wetu na madereva nawambia muwe makini na makundi hayo”
Aliendelea kusema wanawake nao wapewe haki sawa na wanaume katika fursa zitokanazo na ujenzi wa barabara hizo kama vile kujenga mabanda ya biashara, na migahawa kando ya barabara hizo pasipo kubugudhiwa na familia zao na kuepuka ukandamizaji unaofanywa na wanaume kuwakandamiza wanawake katika kujitafutia vipato vya kuinua familia zao
Naye afisa anayeratibu Malalamiko Ndugu. Melleji Molleli akiongea na wananchi katika mikutano hiyo alisema ofisi yake imepokea malalamiko ya wananchi wakilalamika kuhusu vivuko vya barabara kubwa na vinavyoingia katika makazi ya watu, na kusema tayari mkandarasi analifanyia kazi kwa kuweka vivuko hivyo kwa kuanza na barabara ya Kagashe
Alihitimisha kwa kusema marekebisho kwa nyumba zilizoathirika umekuwa ukifanyika , na tayari wiki ijayo wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi watapita kujiridhisha athari zilizojitokeza kutokana na ujenzi wa barabara hizo kwa kata zote na watakuwa wakipiga picha nyumba zote na kulinganisha picha za awali za nyumba zilizopigwa kabla ya mradi kuanza kujengwa
Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji ni moja kati ya Miji saba (7) inayotekeleza mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia(TSCP), miji hiyo ni Arusha, Tanga , Mwanza , Mbeya, Dodoma, Manispaa ya Mtwara Mikindani na Kigoma/Ujiji na barabara zinazojengwa ni barabara ya Kaaya –simu, Mwanga-kitambwe-Mwembetogwa, Kakolwa, Ujenzi-Nazarethi, barabara ya Kagashe, Barabara ya Wafipa-Kagera, Barabara ya Maweni-Burega na Barabara ya kuingia hospitali ya Mkoa ya Maweni, Ujenzi wa mfereji wa maji ya mvua ya Mlole na Katonyanga .
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa