Na Mwandishi wetu
Baraza la Madiwani Manispaa ya Kigoma/Ujiji jana March 1, 2021 liliipongeza ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa kushika nafasi ya kwanza Kimkoa katika ufaulu wa wanafunzi kwa mtihani wa Kitaifa wa kuhitimu darasa la saba uliofanyika Oktoba 2020
Pongezi hizo zilitolewa na wajumbe wa baraza hilo baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya na diwani wa kata ya Mwanga Kusini Mhe. Mussa Maulid kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha robo ya pili mwezi Oktoba hadi Desemba 2020/2021
Akiwasilisha taarifa ya kamati mwenyekiti huyo alisema wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba katika Manispaa hiyo ni wanafunzi 4922 wavulana wakiwa 2409 na wasichana wakiwa 2513 na jumla ya ufaulu ukiwa ni asilimia themanini na sita (86%) , wavulana wakiongoza kwa ufaulu wa asilimia themanini na tisa (89%) na wasichana wakiwa na ufaulu wa asilimia themanini na tatu (83%)
Mwenyekiti wa kamati hiyo aliendelea kusema katika matokeo hayo ufaulu umeongezeka kwa asilimia sifuri nukta tano tisa(0.59%) ukilinganisha na matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2019, na katika kata kumi(10) kwa Mkoa wa Kigoma zilizofanya vizuri kata tatu(03) zilitoka Manispaa ya Kigoma/Ujiji ambazo ni Kata ya Kigoma, Mwanga Kusini, na Rusimbi zikiongozwa na kata ya Makere iliyoshika nafsi ya kwanza Kimkoa inayopatikana Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu
Alihitimisha kwa kusema tayari wanafunzi wote waliofaulu wamejiunga na elimu ya upili katika shule mbalimbali zilizopo Manispaa ya Kigoma/Ujiji na awali wanafunzi mia sita tisini na sita (696) walikosa nafasi kutokana na upungufu wa madarasa na tayari wanafunzi wote wamejiunga na masomo kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa Vyumba vya madarasa
Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Baraka Lupoli akizungumzia taarifa hiyo alipongeza wadau wote wa elimu na kuwashukuru walimu wote kwa jitihada walizozifanya huku akiwataka kuendelea kufanya vizuri na wanafunzi kufikia ndoto za maisha yao kutokana na elimu watakayoipata na wataalamu wa elimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Manispaa kuendelea kushikilia nafasi ya kwanza kwa kuzidi kuongeza asilimia ya ufaulu
Naye mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Mwailwa Pangani alisema serikali kupitia wadau mbalimbali inaendelea kuboresha mazingira ya Ufundishaji na Ujifunzaji kwa shule za Msingi na Sekondari na kwa mwaka huu kulikuwa na Upungufu wa vyumba vya madarasa kumi na tatu (13) kwa shule za sekondari suala lililofanya wanafunzi mia sita tisini na sita (696) kushindwa kujiunga na masomo ya upili kwa wakati na kusema tatizo hilo limetatuliwa kwa kujenga vyumba vya madarasa na wanafunzi wote tayari wameanza masomo
Aliendelea kusema tayari madarasa kumi na sita (16) yamejengwa kupitia mradi wa EP4R na utaratibu wa ukarabati na ujenzi wa madarasa umeanza na unatarajia kuendelea kwa shule zote huku akisema kiasi cha fedha Million ishirini ( 20,000,000/=) zimeingizwa katika akaunti ya kata ya Kagera ili kuanza ujenzi wa chumba cha darasa la kisasa kwa Shule ya Msingi Kagera
Katika Mtihani wa kuhitimu darasa la saba uliofanyika Nchini kote mwezi Oktoba,2020 Jumla ya wanafunzi elfu thelathini na tisa mia saba sitini na moja(39,761) walisajiliwa kufanya mtihani huo ikipata ufaulu wa asilimia sabini na saba (77%) na Mkoa ukishika nafasi ya ishirini(20) Kitaifa na Halmashauri zote za Mkoa huo zikiwa na Ufaulu zaidi ya asilimia Hamsini (50%) ikiwa na maana ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo ni zaidi ya nusu ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa