Na Mwandishi wetu
Wamiliki wa baa na kumbi za starehe Manispaa ya Kigoma/Ujiji jana April 8, 2021 wakiwa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo walijadili Sheria ya mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto chini ya umri wa miaka kumi na nane (18)
Wamiliki hao wakiwa na wadau wengine wa kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili walijadiliana hatua za kuchukua katika maeneo yao ili kutokomeza vitendo vya ukatili vinavyoweza kujitokeza wakiwa katika maeneo yao ya kazi
Afisa ustawi wa Jamii Manispaa ya Kigoma/Ujiji Bi. Agnes Punjila aliwataka wamiliki hao wa kumbi za starehe na baa kuwa wana wajibu wa kuwalinda watoto kwa kuhakikisha hawaonekani katika maeneo hayo baada ya saa moja jioni mara tu baada ya burudani za watoto zinapomalizika
Afisa ustawi wa jamii huyo akifafanua kifungu namba 17 cha sheria hiyo alisema mtoto yeyote haruhusiwi kuingia katika kumbi za starehe, video, na muziki majira ya usiku na kufanya hivyo ni kinyume na sheria hiyo, huku akitoa onyo kwa wazazi na walezi wanaotembea na watoto wao maeneo hayo na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuendeleza ukatili jambo ambalo linaweza kusababisha adhabu na kifungo cha jela kwa wazazi hao
Aliendelea kusema kuwa mzazi ni lazima awajibike kwa kumtunza mtoto kwa kuhakikisha anampatia elimu, malazi , chakula na mtoto kuwa na furaha wakati wote na wazazi hao waepuke kuwaagiza watoto kununua sigara, pombe, na aina yoyote ya kilevi madukani na kufanya hivo ni kukiuka sheria
Afisa dawati la Jinsia na Watoto wa jeshi la Polisi Esther Andrew aliwataka wadau hao waliohudhuria kikao kila mmoja kuwa mlinzi wa mtoto na kuitaka jamii kutoa ushirikiano mara baada ya mtuhumiwa wa vitendo vya ukatili kufikishwa mahakamani na kutoyamaliza kindugu kutokana na athari zinazoweza jitokeza
Afisa huyo alisema vitendo hivyo ni lazima viishe ili kuwa na jamii yenye maadili na kufanya kazi kwa ushiriki wa kila mmoja huku akisema kwa mwezi January hadi February 2021 mimba kumi (10) za utotoni zililipotiwa huku watu watatu (03) wakifikishwa mahakamani kwa kuhusika na vitendo hivyo
Aliendelea kusema katika kuhakikisha vitendo hivyo vya ukatili vinamalizika kila Mwana jamii ana wajibu wa kutoa taarifa za ukatili ambao utafanyika kwa mtoto na mtu yeyote ili mradi awe na ushahidi kuwa haki za mtoto zinakiukwa na wao kama jeshi la polisi wataendelea kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha haki ya mtoto inalindwa
Naye afisa utamaduni wa Manispaa hiyo Ndugu. Abdul Utimbe aliwataka wamiliki wa baa na kumbi za starehe kufanya kazi kwa mjibu wa sheria na kufuata taratibu za vibali wanavyokuwa wakipokea katika sherehe na sikukuu mbalimbali kwa kuhakikisha sherehe za watoto zinamalizika saa moja kamili jioni na kutowaruhusu watoto kuingia katika maeneo hayo majira ya usiku
Mwakilishi kutoka Ngome Urusi Ndugu. John Mlerama alisema wataendelea kupinga vitendo vya ukatili vinavyoweza kufanyika na kuhakikisha watoto hawahudhurii maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi majira ya usiku na hata mda wa masomo ili kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na makundi mbalimbali ndani ya jamii
Kwa kipindi cha mwaka mmoja kamati ya kutokomeza ukatili kwa watoto na wanawake (MTAKUWWA) Manispaa ya Kigoma/Ujiji ilisimamia mashauri ya ukatili wa kimwili kwa watoto kumi (10), watoto waliotelekezwa na wazazi wao mia moja na arobaini na moja (141) na migogoro arobaini na saba (47) ya ndoa ilitatuliwa huku migogoro mingine ikifikishwa mahakamani
Katika kikao hicho wadau mbalimbali waliohudhuria ni wamiliki na waendeshaji wa kumbi za starehe, baa, wamiliki wa kumbi za video na mziki, ngome za mijadala mbalimbali, watendaji mitaa na kata,maafisa maendeleo, Afisa Utamaduni, Maafisa ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa