Wataalamu kutoka Benki ya Dunia (WB) wamefanya ziara ya siku mbili katika manispaa ya kigoma/Ujiji kukagua ubora wa miradi iliyojengwa chini ya mradi wa Uenderezaji wa Miji na Majiji Tanzania(TSCP) huku wakionesha kuridhishwa na kuahidi kuleta miradi mingine katika halmashauri hiyo
Ziara hiyo ilianza jana march 10 na kukamilika leo march 11 ambapo wataalamu hao wameambatana na wataalamu kutoka TAMISEMI ,wataalamu kutoka wizara ya Fedha ,na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri kama wenyeji
Wataalamu hao wametembelea barabara nane(8) za lami zenye urefu wa Km 11.97, dampo la msimba na mifereji ya maji ya mvua ya Katonyanga na Mlole yenye urefu wa Km 2.32 ambapo wameridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo
Akizungumzia ujenzi wa miradi hiyo iliyokamilika Eng. Fredrick Nkya kutoka Benki ya Dunia amesema Mradi huo wa TSCP unatarajia kufungwa May 26, mwaka huu kwa mikoa na halmashauri ambayo inahusika na miradi hii na kuitaka Halmashauri kusimamia maeneo ambayo hayajakamilika katika ujenzi wa barabara hizi
Amesema katika barabara zilizojengwa yapo mapungufu ambayo hayajafanyia kazi na mkandarasi aliyejenga barabara hizo anatakiwa ayakamilishe kabla ya kukabidhi barabara hizo na mda wa mradi kuisha ili kuepusha gharama kwa zinazoweza kujitokeza kwa Manispaa baadae
Amesema mambo ambayo mkandarasi hajayakamilisha katika ujenzi ni pamoja na uwekaji wa alama za barabarani, kukarabati nyumba zilizoathiriwa na mradi kipindi cha ujenzi, kufungwa kwa taa mia moja na kumi(110) ambazo ni nyongeza katika barabara hizo na kuitaka Halmashauri kupitia Kaimu Mkurugenzi kukamilisha upandaji wa miti ya michikichi katika barabara hizo ili kuinua na kuendeleza zao la Michikichi
Naye Mtaalamu kutoka Wizara ya Fedha Eng.Kenneth Nichie ameipongeza halmashauri kwa usimamizi uliofanyika katika miradi iliyojengwa huku akiendelea kuwaasa wataalamu wa Halmshauri kuendelea kusimamia ubora wa kazi ukilinganisha na malipo yanayokuwa yanafanyika kwa miradi inayojengwa
NayeMtaalamu kutoka ofisi ya Raisi Tamisemi Bi.Grace Kyaruzi amewapongeza wageni hao kutoka Benki ya dunia na kuwataka wataalamu wa Halmashauri kuendelea kusimamia na kutekeleza maelekezo yaliyotolewa ili kuweza kuleta tija kwa miradi iliyotekelezwa
Amesema “miradi yetu ya barabara tuliyoijenga hatutaki ije ilete madhara kwa wananchi bali wananchi wafurahie maendeleo yao, hivyo kwa yale yaliyoagizwa kwa Manispaa hebu myatekeleze, yale yanayohitaji kushirikiana na mamlaka zingine fanyeni hivo, shirikianeni na jeshi la polisi (trafiki) ili kuweka alama za barabarani na kuleta furaha ya matumizi ya miundombinu kwa watu wote na rika zote”
Akitoa pongezi zake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Ndugu. Frednand Filimbi amewapongeza wageni hao kutoka Benki ya Dunia na kuahidi kusimamia maelekezo waliyoyatoa katika ziara waliyoifanya na kusema watashirikiana na jeshi la Polisi(Trafiki) kuandaa alama za Usalama barabarani ili kuweza kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza huku akiahidi suala la upandaji michikichi kando ya barabara hizo kufikia mwishoni mwa mwezi march upandaji huo utakuwa umekamilika
Aidha wataalamu hao wametembelea miradi mingine nayotarajiwa kujengwa katika mradi mwingine mpya wa TACTIC unaotariwa kuanza mwezi july baada ya mradi wa TSCP utakapokuwa umefungwa mwezi may mwaka huu
Miradi hiyo mingine waliyotembelea kama rasimu ya awali ni uendelezaji wa ujenzi wa barabara ya wafipa-kagera hadi mto Ruiche ambapo daraja litajengwa kuunganisha eneo la Mgumile, barabara ya Ujiji-Burega –Bangwe, Barabara ya kasulu road kutoka Ujiji hadi Msimba, ujenzi wa Ukumbi mikutano wa kisasa eneo la Mwanga Community Centre, Uendelezaji wa standi ya Malori eneo la Gungu, Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Ujiji na uendelezaji wa ujenzi wa mifereji ya Maji Katonyanga na Mlole kuelekea ziwani
Katika miradi pendekezwa wamemtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kukutana na wadau mbalimbali, vyama vya kisiasa na kupokea maoni ya wananchi kwa miradi mipya itakayojengwa kupitia mradi mkubwa wa TACTIC utakoanza mapema mwezi july.
Manispaa ya Kigoma Ujiji
Sanduku la Posta: S.L.P 44
Simu: +255 28 2802535
Namba ya Simu: +255765660847
Barua pepe: municipal@kigomaujijimc.go.tz ictsecurity@kigomaujijimc.go.tz
Hakimiliki@2017 Manispaa ya Kigoma Ujiji. Haki Zote Zimehifadhiwa